HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 9 October 2018

TAMISEMI yapokea magari mawili kutoka USAID Boresha Afya

 Kaimu Mkurugenzi mkazi wa USAID Tanzania David Thompson (wa tatu kushoto) akimkabidhi mfano wa funguo wa gari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo(katikati) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi magari mawili kwa Wizara hiyo leo Jijini Dar Es Salaam. Wa kwanza kulia ni Dk. Marina Njelekela, Wa Tatu kulia ni Mkurugenzi wa Deloitte Consulting LTD, Carlton Jones na wapili kulia ni Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI Dkt Zainabu Chaula.
Na Mathew Kwembe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amepokea magari mawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 na kusema kuwa magari hayo yataongeza thamani katika juhudi za serikali za kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Akiongea katika hafla ya makabidhiano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa USAID Tanzania David Thompson aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira yake ya kuboresha viwango vya afya kwa watanzania wote.
“Kupitia msaada huu, Serikali ya Marekani inaungana na Serikali ya Tanzania kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote, katika jamii za watu wa Lindi na Mtwara, mkazo zaidi ukiwa kwa wanawake na vijana,” alisema.
Kabla ya kuyapokea magari hayo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) David Thompson, Waziri Jafo alisema kuwa anatambua kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Marekani kupitia Mradi wa USAID Boresha Afya kanda ya kusini.
Alisema kuwa kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na mradi wa Boresha Afya katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara na Ruvuma anayo furaha kubwa kushiriki katika hafla hiyo ya kupokea magari hayo yenye thamani ya Tsh.219, 372,136.
“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania ningependa kuwafikishia shukrani zetu za dhat kwa Serikali ya Marekani na wote walio katika mradi huu wa USAID Boresha Afya Kanda ya kusini,” alisema.
Waziri Jafo aliongeza kuwa serikali inajivunia kushirikiana na washirika ambao kweli wanajali hali za raia wa Tanzania.
Alisema kuwa kupitia msaada huo USAID Boresha Afya Kanda ya kusini imeonyesha kweli iko pamoja na watanzania katika kusimamia changamoto za afya nchini.
Waziri Jafo alitoa wito kwa Wakuu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuhakikisha kuwa magari hayo yanatunzwa kwani hiyo itawatia moyo washirika wa maendeleo kuendelea kutoa misaada zaidi.
Aidha Waziri Jafo alisema Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini katika kipindi cha miezi 12 iliyopita imefanikiwa kukamilisha vituo vya afya 210 na hivyo inasubiri kupatiwa madawa kutoka bohari kuu ya madawa nchini.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miezi 18 ijayo Serikali inatarajia kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya 340 ambapo vituo 100 vitaweza kutoa huduma ya upasuaji.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt.Zainab Chaula aliishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada huo wa magari na kuongeza kuwa msaada huo utajazia juhudi za serikali katika kuboresha huduma za Afya nchini.
Alisema kuwa magari hayo yatatumiwa na Timu ya Usimamizi wa Afya katika Mikoa ya Lindi na Mtwara katika kusaidia na kuimarisha usimamizi wa shughuli zinazohusiana na VVU, uzazi wa mpango, Kifua Kikuu, Malaria, lishe, jinsia, Jamii na nyinginezo zinazohusiana na afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara DKT Wedson Sichalwe na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi DKt Genchwele Makenge waliishukuru serikali ya Marekani kwa msaada huo kwani unakwenda sambamba na malengo ya serikali ya kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Mradi wa USAID Boresha Afya Kanda ya Kusini ni mradi wa miaka mitano ulioanza oktoba 2016 na unatarajia kukamilisha shughuli zake ifikapo mwezi septemba mwaka 2021 unaotekelezwa na halmashauri 43 kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa kushirikiana na mashirika ya kitaalamu ya FHI na EngenderHealth na Management and Development for Health (MDH)
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo akizungumza wakati wa kupokea msaada wa magari mawili katika wizara hiyo yatakayotumika katika mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia mradi wa USAIDS Boresha Afya Kanda ya Kusini.
 Kaimu Mkurugenzi mkazi wa USAID Tanzania David Thompson akizungumza kuhusu wanavosimamia miradi mbalimbali ya USAID hapa nchini Tanzania wakati wa hafla fupi ya kukabidhi magari mawili kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Mkurugenzi wa Deloitte Consulting LTD, Carlton Jones akizungumza kuhusu wanavyosimamia mradi wa USAID Boresha Afya kanda ya Kusini unaotekelezwa katika halmashauri 43 kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma wakati wa kutoa msaada wa magari mawili kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo akiwasha moja ya gari mara baada ya kukabidhiwa magari hayo mawili yatakayotumika  kwenye kuimarisha usimamizi wa Shuguli zinazohusiana na masuala ya Afya katika mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia mradi wa USAID Boresha Afya Kanda ya Kusini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo(kulia) akimkabidhi mfano wa funguo ya gari  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Wedson Sichalwe(kushoto) ili kusaidia na kuimarisha usimamizi wa Shughuli zinazohusianana na VVU, Uzazi wa mpango. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi mkazi wa USAID Tanzania David Thompson 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo(kulia) akimkabidhi mfano wa funguo ya gari  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk. Genchwele Makenge(kushoto) ili kusaidia na kuimarisha usimamizi wa Shughuli zinazohusianana na VVU, Uzazi wa mpango. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi mkazi wa USAID Tanzania David Thompson 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kukabidhiwa magari mawili na USAID kupitia mradi wa USAID Boresha Afya kanda ya Kusini unaotekelezwa katika halmashauri 43 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma.


Baadhi ya wageni waalikwa wakiwa kwenye hafla fupi ya kukabidhi magari mawili kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
  Magari yaliyotolewa na USAID kupitia mradi wa USAID Boresha Afya kanda ya Kusini  yatakayosaidia masuala ya Afya katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad