HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 25, 2018

PRECISION AIR YAFANYA MAFUNZO YA USALAMA WADAU WA SEKTA YA ANGA

SHIRIKA  la Ndege laPrecision Air  likishirikiana na Taasisi ya kimataifa ya Usafiri wa anga (IATA)) wameandaa mafunzo ya usalama wa anga yatakayofanyika kwa kipindi cha wiki 4 kwa wadau wa sekta ya  anga Tanzania.

Mafunzo hayo yatakayokuwa katika awamu tofauti yataendeshwa na mkufunzi maalum wa IATA kutoka Ufaransa, na yalianza Jumatatu Tarehe 22 Oktoba 2018 na itafikia kikomo  Ijumaa tarehe 2 Novemba 2018 huku  awamu ya pili ikitarajiwa kuanza Tarehe 14 mpaka tarehe 21 Novemba 2018.

Mafunzo hayo yatajikita kwenye masomo ya usalama wa anga katika nyanja tofauti zikiwemo masomo ya awali ya utekelezaji wa usimamizi wa mfumo wa usalama, usimamizi wa usalama, pamoja na kuwaandaa wakufunzi wapya wtakaotumika kuwaelimisha wafanyakazi wenzao katika maeneo yao ya kazi. 

Precision Air pia imewaalika washiriki kutoka shirika la Ndege la  Air Tanzania pamoja na FastJet.

Mkuu wa Idara ya usimamizi wa Ubora, Usalama na Ulinzi Precision Air Patrick Mwanri amesema kwamba mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kujenga  utamaduni wa kuzingatia usalama katika maeneo yao ya kazi huku wakiboresha utendaji wa Precision Air, Air Tanzania na FastJet na kuiwezesha Precision Air kukidhi viwango vya kimataifa vya usalama, ambavyo vinaitaka Precision Air kufanya mafunzo maalumu kwa wafanyakazi wake, katika kutekeleza Mfumo wa Usimamizi wa Usalama.

Pamoja na kutimiza matakwa ya viwango vya kimataifa, lakini pia wamewaalika wadau wengine wa usalama kutoka Air Tanzania pamoja na Fastjet ili tuweze kupata maarifa haya kwa pamoja ili tuweze kuimarisha hali ya usalama katika sekta ya anga, kwani swala la usalama halina ushindani, pia wakati huo huo tukiendelea kuunga mkono juhudi za Serekali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Mh.Raisi Dkt.Joseph Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya anga nchini. Anga letu likiwa salama, watalii na wafanya biashara watatuamini zaidi na kuendelea kuttembelea nchi yetu na kutumia mashirika yetu ya Ndege. Aliongeza Bw. Mwanri.

Precision Air ni shirika la ndege pekee ambalo ni mwanachama wa IATA hapa Tanzania. Ili kukidhi viwango vya utendaji vya kimataifa, Precision Air hutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake mara kwa mara kwa lengo la  kuwaongezea maarifa mapya  ya usimamizi wa usalama katika sekta ya anga.

Kama Shirika linalozingatia viwango vya kimataifa, kwa nyakati tofauti Precision Air imeitoa Tanzania katika kaguzi mabali mbali za usalama wa sekta ya anga, zinazofanywa na mamlaka za kikanda na kimataifa kama ICAO na IATA.

Shirika la Ndege la Precision Air lilianzishwa mwaka 1993 kama shirika binafsi la ndege za kukodi, likifanya safari zake kusafirisha watalii katika vivutio vya utalii kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro pamoja na Visiwa vya Zanzibar. Sasa Shirika hilo lenye makoa yake makuu katika Jiji la Dar es Salaam limeendelea kukua na kuwa moja ya mashirika yanayo heshimika katika ukanda wa Africa Mashariki na Africa kwa ujumla.Ikifanya safari zake kutokea Dar es Salaam, Precision Air inasafiri kuelekea Arusha, Bukoba, Kilimanjaro, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kahama, Zanzibar,Nairobi na Entebbe. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad