HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 27 October 2018

MAKAMU WA RAIS AWATAKA WANANCHI KULINDA MIUNDO MBINU YA MAJI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akizungumza wakati wa ziara yake ya Mkoa wa Pwani baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tenki la maji la Kisarawe lenye uwezo wa kuhifadhi Lita Milioni sita kwa siku na kuupongeza uongozi wa DAWASA kwa kazi nzuri wanayofanya Leo Wilaya ya Kisarawe.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan Suluhu amewataka wananchi wa Kisarawe kulinda miundo mbinu ya maji ili iwapatie maji safi na salama.

Mama Samia ameyasema hayo wakati akitembelea  mradi wa ujenzi wa tenki la maji la Kisarawe  lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita Milioni sita kwa siku.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo,  Mama Samiaa ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kwa hatua kubwa wanayoifanya ya kutimiza azma ya mkoa wa Pwani kupata maji safi na salama.

Amesema kuwa, pongezi pia ziende kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji inayoongozwa na Profesa Makame Mbarawa kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika kabisa sio tu Dar es salaam na Pwani bali Tanzania nzima.

Mama Samia amesema kuwa, kumekuwa na miradi kusuasua  ila kwa usimamizi wake wa Waziri wa Maji utaenda vizuri na maji yatapatikana.

"Kuja kwa mradi huu mkubwa wa maji utawapatia vijana ajira katika viwanda baada ya wawekezaji kuja na najua umeme upo na wa gesi unakuja,"amesema Mama Samia.

Kwa upande wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa amesema  mradi huu utagharimu bil 10.04 na fedha zote zitalipwa na DAWASA baada ya kukubaliana kwa mamlaka hizi kujiendesha zenyewe.

Mbarawa amesema kuwa mradi huu utakuwa chini ya kampuni ya Chico na utadumu kwa miezi minane na kufikia Julai 2019 utakuwa umekamilika na pia kutakuwa na ujenzi wa bomba la Km 5 kwenda Vigungu na Km 14 kwenda Viwandani, kujenga tenki litakalohifadhi maji Lita 480 na pampu nne kubwa na wananchi wa Kisarawe kupata maji kwa asilimia 100.

Katika kutekeleza miradi mbalimbali ya DAWASA imetengwa akaunti maalumu ambapo asilimia 30 ya mapato inawekwa kwenye akaunti hiyo kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa ana imani na DAWASA mpya na maji yatakuja Mkoa wa Pwani na uwepo wa mradi huu hali ya upatikanaji wa maji itabadilika. 

Amesema kuwa Serikali ya mkoa itatoa msaada kwa kandarasi ili maji yafike ikiwemo kutoa vibali mbalimbali kwa ajili ya kupitisha mabomba ya maji na kuna maeneo ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda ulikua unasuasua kwani walikuwa wakihitaji maji ila kwa sasa watakuja baada ya maji kufika Kisarawe.

Naye Waziri wa TAMISEMI na Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo ameshukuru kwa mradi wa maji kufika Wilaya ya Kisarawe na kupitia mradi huu wana kisarawe watakuwa wamenufaika kwa asilimia kumi.

Ameyataja maeneo ya Mzenga na Mwanalumango kuwa na shida kubwa ya maji na watu wa Kisarawe wanaishukuru sana serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kufanikisba mradi huu kwani ni mara ya kwanza toka kupata kwa uhuru.

Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Selemani Jafo akizungumzia mradi wa ujenzi wa Tenki la maji la Kisarawe lenye uwezo wa Kuhifadhi maji Lita Miliono sita kwa siku kuwa utawanufaisha Wananchi wa Kisarawe na kupata maji safi na salama kwa uhakika zaidi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akimuelezea Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu mradi wa ujenzi wa tenki la maji linalojengwa Kisarawe wakati wa ziara yake Leo.
 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Mbarawa akielezea jambo kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu wakati wa ziara yake ya Mkoa wa Pwani na kutembelea mradi wa ujenzi wa tenki la  maji la Kisarawe lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita kwa siku.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Samia Suluhu katika Wilaya ya Kisarawe leo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian  Luhemeja wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu alipotembelea mradi wa ujenzi wa tenki la Maji lenye uwezo wa kuhifadhi maji Lita Milioni sita kwa siku.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad