HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 8 October 2018

DED BAGAMOYO APANGA VIKOSI KAZI KUFUATILIA VYANZO VYA MAPATO ILI KUONGEZA MAPATO YA NDANI

NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO

HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo, imeanza kusambaza vikosi kazi vya wataalamu ambao watatembelea na kufuatilia vyanzo vya mapato yake ya ndani kujua changamoto zinavyovikabili ili kufikia asilimia 25 ya makusanyo kwa kila robo ya mwaka .

Aidha halmashauri hiyo, imetumia milioni 20 ya mapato yake na nguvu za wananchi ,kujenga makalavati makubwa matatu kata ya Kilomo ,hatua iliyosaidia kupitika kwa barabara na kuongeza mapato ya chanzo cha machimbo ya mchango .

Akielezea walivyojipanga katika eneo la ukusanyaji wa mapato ,mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ,Fatuma Latu ,alisema ,wamekubaliana kuwe na vikosi kazi kufuatilia japokuwa wapo wakusanya mapato ,kodi kwenye kata .

Alisema, itawezesha kwenda pamoja na mpango mkakati wa kimkoa wa Pwani ,kuwa kila robo ya mwaka kukusanya asilimia 25 na kama usipofikia utoe changamoto halisi iliyosababisha kutofikia lengo hilo .

Latu alieleza ,moja ya majukumu yao ni kuhakikisha halmashauri inakusanya mapato kwa kiasi kikubwa kulingana na vyanzo vya mapato .

"Mwaka Jana tuliunda kikosi kazi cha kutambua vyanzo baada ya kugawanyika Bagamoyo na Chalinze "

"Kilichofuata sasa ni kununua mashine za kutosha (posi )kwa ajili ya ukusanyaji mapato ,kutoa elimu kwenye mikutano ya maeneo na madiwani na wenyeviti wa vitongoji kushirikiana kusimamia ukusanyaji wa mapato na kodi,"alibainisha Latu .

Alifafanua kwa asilimia kubwa wanategemea chanzo cha mchanga katika kata ya Kilomo ambayo ndio yenye vibali hivyo.

Alieleza kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 walipata changamoto kubwa ya mapato madogo kwenye eneo hilo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kutoa makalavati makubwa matatu .

"Tunalitegemea sana eneo hilo kuinua mapato yetu ,mwaka jana tuliyumba ,na bahati mbaya hakukuwa na fedha iliyoelekezwa kutengeneza barabara hiyo kupitia TARURA "alieleza Latu

"Kwahiyo tuliamua na kujitahidi kutoa fedha za mapato ya ndani na nguvu za wananchi ,hivyo tunatarajia mapato yatapanda na kurudi kwenye hali yake kwenye chanzo hicho "alisema .

Kwa mujibu wa Latu , vyanzo vingine wanavyovitegemea kuongeza mapato ya ndani ni soko la samaki huko feri ya Bagamoyo na stendi .

Diwani wa kata ya Kilomo Hassan Wembe ,alisema chanzo kikuu kinachoongoza cha mapato ni ushuru wa mchanga na kata inayoongoza kwenye chanzo hicho ni Kilomo na Yombo .

Alisema kawaida kwa mwezi makusanyo  hayo hufikia sh .mil 80 kwa mwezi ambapo kwenye robo ya mwaka hupatikana hadi sh.milioni 280 lakini kwa mwaka jana kilishuka kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu kutokana na mvua .

Nae diwani wa kata ya Yombo Mohammed Usinga alisema ,watashirikiana na halmashauri kuhakikisha wanaimarisha na kuboresha mapato .

Usinga, alisema watasimamia na miradi ya maendeleo na fedha za umma ndio maana wamepata hati safi .

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainab Kawawa alitoa rai kwa wataalamu ,madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kuwa wamoja na kushirikiana ili kuleta maendeleo chanja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad