HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 8, 2018

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AKABIDHI SOLAR POWER KWA ZAHANATI TATU ZA HALMASHAURI YA CHALINZE

Na Victor  Masangu, Chalinze
WANAWAKE  wa kijiji cha Mduma  kata Magindu  katika halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani  kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na nishati ya umeme hivyo inawalazimu kupatiwa matibabu  kwa kutumia mwanga wa tochi au simu  pindi wanapokwenda kujifungua  katika zahanati ya Mduma  kitu ambacho ni hatari kwa usalama wa maisha yao.

Wakizungumza   kijijini hapo  kuhusiana na changamoto inayowakabili wanawake hao wamesema   kwamba kwa sasa  wanapata shida kubwa wakati wa kujifungua hasa katika nyakati za usiku kutokana na kuwa na giza hivyo kuwapa wakati mgumu  wauguzi  pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Aidha walisema  kwamba kwa kipindi kirefu katika zahanati hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbali mbali za upatikanaji wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa hivyo wameiomba serikali ya awamu ya tano kuingilia kati suala hilo kwa lengo la kuweza kuwafikishia nishati ya umeme ambayo itakuwa ni mkombozi katika utoaji wa huduma hasa katika nyakati za usiku.

Kwa upande wake mmoja wa wauguzi katika zahanati ya Mduma Neema Muhagama amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya kutokuwa na nishati ya umeme hivyo inawapelekea  wakati mwingine kutumia mwanga wa tochi  za simu katika kuwapatia matibabu wagonjwa hasa kwa upande wa wakinamama wajawazito pindi wanapohitaji kujifungua.

Katika kuliona hilo Naibu  Waziri wa nishati Subira Mgalu  ambaye amefanya ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya umeme vijijini  ametoa Solar Power  sita katika zahanati tatu tofauti ambazo ni Kwamduma,kibindu pamoja na Kwamsanja kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa nyakati za usiku, huku akibainisha  serikali tayari  imeshaanza  kupeleka umeme  vijiji  kupitia mradi wa REA awamu ya tatu ili kuwaondolea adha wananchi ambayo wamekuwa wakipata kwa kipindi  kirefu.

 Mgalu alisema kwamba lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na nishati ya umeme kupitia Mradi wa  Rea kwa lengo la kuweza kuboresha huduma mbali mbali pamoja na kuwaondolea kero ambayo wamekuwa wakiipta wananchi kwa kipindi kirefu.

“Mimi  nikiwa kama Naibu waziri wa nishati pamoja na Mbunge wa viti maalumu kutoka Mkoa wa pwani nimefanya ziara yangu kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya umeme lakini nimekutana na  changamoto  nyingi lakini kubwa zidi nimejionea baadhi ya zahanati wakinamama wajawazito na wagonjwa wengine wanapatiwa matibabu kwa kutumia mwanga wa tochi,hivyo nikaamua kwa kuanzia nitoe solar power ili ziweze kuwasaidia kwa sasa wakati wakisubilia umeme wa uhakika,”alisema Mgalu.

BAADHI ya  zahanati zilizopo katika halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani  zimekuwa zikikabiliwa na changamoto  mbali mbali ikiwemo kukosa huduma ya uhakika ya nishati ya umeme hivyo kupelekea baadhi ya wauguzi na madaktari kuamua kutumia mwanga wa simu au tochi kwa ajili ya kuwamulikia wagonjwa ili kuwapatia matibabu.
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu wa katikati ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu (CCM) kutoka Mkoa wa Pwani  akikabidhi msaada wa Solar Power  kwa baadhi ya wauguzi wa zahanati ya Mduma iliyopo kata ya Kibindu  katika halmashauri ya Chalinze iliyopo Wilayani Bagamoyo   kulia kwake ni muuguzi Neema Muhagama akipokea kwa niaba ya wenzake.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
 Naibu Waziri wa nishati Subila Mgalu wa kulia ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu (CCM) kutoka Mkoa wa Pwani akimkabidhi msaada wa Solar Power  Martha Kilimba ambaye ni mmoja wa wauguzi  katika zahanati ya Kwamsanja iliyopo kata ya Kibindu katika halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa ambao wamekuwa wakipata adha ya kutibiwa kwa kutumia mwanga wa tochi za simu.
Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu kulia ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu (CCM) kutoka Mkoani Pwani akimkabidhi msaada wa Solar Power mmoja wa wauguzi katika zahanati   ya Kibindu iliyopo kata ya Kibindu katika halmashauri ya Chalinze iliyopo Wilayani Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad