HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 26 October 2018

AFISA TARAFA ITISO ATANGAZA KIAMA KWA WAVAMIZI WA MAENEO YA MALISHO

AFISA Tarafa wa Itiso  Remidius Emmanuel ametangaza vita kwa watu wote waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Malisho  katika Tarafa hiyo iliyopo wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Remidius amesema hayo mapema wiki hii  katika mkutano maalumu wa kujibu kero mbalimbali katika  kijiji cha Gwandi na kuhusisha  Wafugaji kutoka kata ya Zajilwa. 

Akisoma taarifa mbele ya Afisa Tarafa, Katibu wa Chama Cha Wafugaji Wilaya ya Chamwino Bw. Reginaldo Lubeleje alitaja baadhi ya  Changamoto wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa  malisho,njia za mifugo, upungufu wa Majosho ya Mifugo, Mahusiano madogo kwa baadhi ya  Viongozi wachache wa  Serikali na Chama cha Wafugaji.

Imeelezwa kuwa baadhi ya maeneo katika Tarafa ya Itiso  yalitengwa kabisa kwa ajili ya Wafugaji lakini yamevamiwa na Wakulima wakubwa na baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na Mbuga ya Yobo, Uliuli,Dongo, Jelesa, Mazuguni na Haneti  hizi mbuga zilitengwa kwa ajili ya malisho ila maeneo hayo yamevamiwa na wakulima wakubwa.

Akieleza mafanikio yao katibu wa chama cha wafugaji Iti amesema kuwa;  chama hicho kimefanikiwa kuwaunganisha Wafugaji  wote bila kujali Ukabila, dini na Itikadi ya mtu, mbali na kuweza kutatua baadhi ya matatizo yao wenyewe  wamefanikiwa pia  kushiriki katika vikao mbalimbali vilivyo husisha Makundi ya Wafugaji aidha wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga kwa kuendelea kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Wilaya ya Chamwino.

Akijibu kero hizo Afisa Tarafa Remidius Emmanuel amesema kuwa, uwezekano wa kuibuka  kwa migogoro ya Wakulima na Wafugaji  wakati mwingine hutokana na uzembe wa baadhi ya viongozi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.

Amesema kuwa; "Sasa unakuta kiongozi anafahamu kabisa kwamba haya maeneo yametengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo, alafu anaona yanavamiwa alafu yeye amenyamaza tuu, na ninazo taarifa kuna baadhi ya viongozi wa  Serikali za Vijiji ambao wameshiriki kuuza maeneo hayo, Wajiandae kuyarejesha kabisa na zoezi hili litafanyika Tarafa nzima.Kwa hiyo kama kuna watu wamejimilikisha maeneo hayo wambieni wayarejeshe  haraka.Watatueleza nani aliwauzia na ni kwa utaratibu upi? na katika hili sitorudi nyuma, ni jukumu letu viongozi kutatua migogoro na sio kuwa sehemu ya Migogoro" Amesem Remidius.

Hata hivyo amewaeleza kuwa licha ya juhudi za Serikali katika kutatua kero ya  Majosho ya mifugo lakini amewataka Wafugaji kupokea ushauri kutoka kwa  wataalamu wa Mifugo  ili kuepuka Magonjwa mbalimbali yanayoweza kuipata mifugo yao.

Aidha amesema kuwa, "Ni kweli ipo Changamoto ya Majosho kwa ajili ya Mifugo yetu, lakini baadhi ya  Serikali za Vijiji na Kata  wamefanikiwa kutatua kero hii kwa kuwatumia Mawakala na Makundi ya wafugaji  lakini nasisitiza ili kufanikisha taratibu hizo nimewaelekeza kushirikisha Wataalamu wetu wa Halmashauri, lakini ninazo taarifa pia baadhi yetu  sisi Wafugaji bado hatuna muamko wa kupeleka Mifugo yetu katika Majosho yaliyopo, niombe uongozi wa Chama cha Wafugaji kuhimiza umuhimu wa kutekeleza ushauri wa Kitaalamu ili Mifugo yetu isishambuliwe na magonjwa" Amesema Remidius.

Na amesema kuwa suala la mahusiano ni muhimu kwa makundi yote katika Tarafa hiyo na,ataendelea kuwahimiza viongozi  kuimarisha mahusiano na makundi yote ikiwemo Wafugaji, na amewashukuru wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za Maendeleo.

"Juzi nimeshuhudia  Wafugaji wa Kijiji cha Nayu kata ya Dabalo kwa hiari yao mwenyewe wameamua kuchangia ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji hicho nimefurahi sana" Ameongeza   

Hata hivyo Afisa  Tarafa ameziagiza Serikali za vijiji vyote katika Tarafa ya Itiso kupitia kamati husika kusimamia suala la njia za Mifugo, huku akisisitiza kwamba kukosekana kwa njia hizo kumechangia pia uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Na amehitimisha kwa  kusema kuwa wafugaji na Wakulima wote wanategemeana na yeye kama kiongozi wa Tarafa hiyo  ataendelea kusimamia mipango mizuri inayotoa haki kwa makundi yote kuishi bila migogoro na kuwataka wafugaji  pia kutoa ushirikiano katika jamii kwa kuheshimu sheria na taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuepuka migongano kwa kuingiza  mifugo katika mashamba halali ya Wakulima hatua ambayo imekuwa ikijitokeza kwa baadhi ya maeneo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha wafugaji kanda ya kati Neema Ally amempongeza Afisa Tarafa kwa kuonyesha dhamira ya kutatua Changamoto zinazowakabili wafugaji hao  na kuhimiza umuhimu wa serikali za vijiji kuendelea na utaratibu wa mipango itakayo ainisha maeneo ya malisho  na huduma nyingine za mifugo ili kuondokana na migogoro inayoweza kujitokeza baina ya Wafugaji na wakulima.
 Afisa Tarafa wa Itiso Remidius Emmanuel akizungumza na Wafugaji katika mkutano maalumu wa kujibu kero mbalimbali kijiji cha Gwandi na kuhusisha Wafugaji kutoka kata ya Zajilwa.
 Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji kanda ya kati, Neema Ally akizungumza na wafugaji  wakati wa mkutano huo uliofanuka katika kijiji cha Gwandi kata ya Zajilwa.
Baadhi ya wafugaji wakiwasilisha kero zao mbele ya Afisa Tarafa

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad