HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 28, 2018

VIONGOZI WA KIJIJI WAFUNGA OFISI, “WATIMKA” KISA OPERESHENI YA BHANGI

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wananchi wa kijiji cha Kisimiri Juu Kilichopo tarafa ya King’ori wilayani Arumeru walikiacha kijiji chao kwa muda huku viongozi wao wakifunga ofisi zao na kukimbia kisa operesheni ya bhangi iliyofanywa na vikosi vya Jeshi la Polisi. 

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema kwamba walitapata taarifa kwamba kuna kiasi kikubwa cha bhangi kinatarajia kusafirishwa ndipo walipoandaa askari hao ambao walifanikiwa kufika eneo la tukio na kupata jumla ya magunia 27 yenye uzito wa Kilogramu 25 kila gunia shambani kwa mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa pamoja na Misokoto 583 ya Bhangi.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba kwa sasa Jeshi la Polisi mkoani hapa linawatafuta viongozi wa kijiji cha Kisimiri Juu kwa kukiuka agizo la Serikali linalomtaka kila kiongozi katika eneo lake ahakikishe kwamba halilimwi bhangi.

“Tunaendelea kuwatafuta viongozi wa kijiji pamoja na kamati zake za ulinzi na usalama na mkondo wa sheria utachukua nafasi kwani wao kama viongozi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha katika eneo lao hakuna biashara yoyote ya Madawa ya kulevya inayofanyika”. Alifafanua Kamanda Ng’anzi.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba Jeshi hilo mkoani hapa lipo makini na litaendelea na mapambano dhidi ya Madawa ya kulevya katika maeneo mbalimbali na kubainisha kwamba katika eneo la mpaka wa Namanga matukio ya uingizaji wa madawa umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni  wa Jeshi hilo mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP) Elias Mwita alisema kwamba  operesheni hiyo sio ya kwanza kufanyika katika eneo hilo na itakuwa endelevu kuhakikisha kwamba zao hilo haliendelei kulimwa.

Si mara ya kwanza kwa viongozi pamoja na wananchi hao kutotoa ushirikiano kwa Jeshi hilo pamoja na vyombo vingine vya usalama pindi wanapofanya operesheni ya bhangi katika eneo hilo ambapo huwa wanaacha makazi yao na kukimbilia milimani.
 Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi
 Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakihesabu misokoto ya Bhangi iliyopatikana katika moja ya nyumba ya wakazi wa kijiji hicho katika operesheni iliyofanyika katika kijiji cha Kisimiri Juu kilichopo tarafa ya King'ori wilayani Arumeru.
Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Elias Mwita akiwaonyesha waandishi wa habari misokoto ya bhangi iliyopatikana katika operesheni hiyo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad