HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 11, 2018

ULAJI USIOFAA UNAONGEZA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesemalishe duni pamoja na ulaji usiofaa na mitindo ya maisha vinachangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususan kwa vijana na watu wazima, ambao ndiyo nguvu kazi kwa Taifa.

“Ni jambo lisilopingika kuwa hatua za kukabiliana na magonjwa ya kusendeka (mfano matatizo ya moyo, saratani, kisukari na shinikizo kubwa la damu) zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kasi ya maendeleo yetu kwani gharama za matibabu yake ni kubwa mno; si kwa kaya zinazoathirika tu bali kwa Taifa zima.”

Waziri Mkuu  ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 11, 2018),  wakati akifungua mkutano wa tano wa wadau wa masuala ya lishe, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema lishe iliyozidi inadhihirishwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukizwa yanayotokana na mabadiliko ya mitindo ya maisha na ulaji usiofaa kama vile uzito uliozidi, viriba tumbo, shinikizo la damu pamoja na kisukari.

Amesema kasi ya ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza inapaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha. “Huu ni wakati wa kuangalia kwa pamoja kama jitihada zetu zinaleta matunda tunayotarajia.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya Taifa letu hivyo, uwepo wao katika mkutano huo unaonesha umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa kila sekta, kila mdau ikiwemo sekta binafsi kwa nafasi yake katika kupambana na aina zote za utapiamlo.

Amesema ushiriki wa kila sekta ni wa muhimu kwa sababu hakuna sekta moja pekee inayoweza kuondoa tatizo la utapiamlo, pia ni vema kwa wadau hao wakajitathmini mmoja mmoja katika sekta zao kuona kama wanaelekea katika muelekeo sawa na mipango ya Serikali.

“Kwa kuzingatia hilo, ofisi yangu imeweka utaratibu maalum wa kuratibu utekelezaji wa kazi za lishe nchini, ambapo kamati ya Kitaifa ya Usimamizi na Ushauri kuhusu masula ya lishe nchini yaani High Level Steering Committee on Nutrition imeundwa ili kusimamia utekelezaji wa azma hiyo.”

Waziri Mkuu amesema kwamba watu wote wanatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kupambana na matatizo ya lishe nchini, ambapo taarifa za wataalamu zinasema kuwa kwa sasa nchi inakabiliwa na aina mbili za utapiamlo yaani lishe duni na lishe iliyozidi au iliyokithiri.

Amesema walengwa wakubwa wa lishe duni ni pamoja na watoto chini ya miaka mitano, wanawake walio katika umri wa kuzaa hususani wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na vijana balehe (hususan wa kike). “Hii ni kwa sababu mahitaji ya virutubishi kwa ajili ya miili yao ni makubwa, ukilinganisha na ule unaohitajika na makundi mengine.”


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na washiriki wa mkutano wa tano wa kutathmini utekelezaji wa afua za lishe nchini, katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Septemba 11, 2018.  

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza na washiriki wa mkutano wa tano wa kutathmini utekelezaji wa afua za lishe nchini, katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Septemba 11, 2018.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Phaustine Ndugulile kushoto na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega kulia, wakifuatilia mkutano wa tano wa kutathmini utekelezaji wa afua za lishe nchini, uliyofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Septemba 11, 2018. 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kabla ya kufungua mkutano wa tano wa kutathmini utekelezaji wa afua za lishe nchini, kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Septemba 11, 2018.


 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia maharage ya lishe, baada ya kufungua mkutano wa tano wa kutathmini utekelezaji wa afua za lishe nchini, kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Septemba 11, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad