HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 13 September 2018

Serikali ituunge mkono wawekezaji-Mulokozi

“Rais John Magufuli amekuwa akitangaza kila wakati kuwa serikali yake ni serikali ya viwanda, hivyo viongozi wa serikali wanapaswa kutuunga mkono sisi wawekezaji na siyo kutukandamiza kwani tunalipa kodi pindi tukizalisha bidhaa zetu na kuziuza, tunawalipa mishahara wafanyakazi wetu na pia sisi wenyewe kama kampuni tunanufaika kupitia uwekezaji tulioufanya, tunanufaika wote,” hivi ndivyo anavyoanza kuzungumza mkurugenzi wa kiwanda cha pombe kali cha Mati Super Brands Ltd cha mjini Babati mkoani Manyara, David Mulokozi.

Mulokozi anasema kuna mamlaka zinapaswa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji tangu awali, wanapoanzisha kiwanda na kuwapa elimu juu ya nini wanapaswa kufanya na siyo kusubiri mara baada ya kuanza uzalishaji wanajitokeza na kudai kuwa wamekosea hivyo watozwe faini na kufungia uzalishaji bila sababu ya msingi.

Anasema mamlaka za serikali zilizopo kisheria ikiwemo mkemia mkuu wa serikali, mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) mamlaka ya mapato nchini (TRA) na shirika la viwango nchini (TBS) zinapaswa kutoa elimu kwa wawekezaji ili wafuate hatua zinazopaswa kufuatwa pindi wanapotaka kuanza uwekezaji ili waeleweshwe juu ya mchakato huo.

Anasema TRA ndiyo mamlaka ya mwisho kutoa kibali cha kufanya shughuli za biashara nchini hivyo walisikitishwa kiwanda chao kufungiwa na mamlaka nyingine bila sababu za msingi ili hali walikuwa wanalipa kodi serikali na walifuata hatua zote zinazotakiwa.

“Tangu tuanze kufanya shughuli kwenye hiki kiwanda chetu hatujawahi kulipa kodi TRA chini ya shilingi milioni 30 kwa mwezi na pia tumesababisha kuwepo kwa ajira kwa wananchi wa mkoa wa Manyara hivyo wakati kiwanda kilipofungwa kwa miezi mitatu watumishi wetu pia waliathirika kwani walikosa kazi kwa muda huo,” anasema Mulokozi.

Anasema kutokana na sera nzuri za Rais John Magufuli waliamua kuanzisha kiwanda hicho wakati ambapo kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda iliposhika kasi illi kuunga mkono kauli mbiu hiyo hivyo wanatakiwa kuungwa mkono kwani miongoni mwa viwanda vilivyoanzishwa kipindi cha utawala wake ni kampuni ya Mati Super Brands Ltd.


Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara
Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alipokitembelea kiwanda hicho anasema hakubaliani na sababu zilizotolewa hadi kusababisha kufungwa kwa kiwanda hicho tangu mwezi Machi mwaka huu alipotoa amri ya kukifungua hivi karibuni.

Mnyeti anasema mwekezaji huyo amefunga mitambo yake na kutoa ajira kwa wananchi wa Manyara, badala ya kupewa ushirikiano na watendaji wanaohusika, wanawakwamisha kwa kukifunga kwa miezi mitatu, bila sababu za msingi.

"Bado kuna watu wamelala wanaandaa mazingira ya rushwa, yaani badala watumie hata siku tatu za kumshauri kitaalamu wanakimbilia kufunga kiwanda kwa sababu ambazo hazina mashiko na zisizo za kitaalamu," anasema Mnyeti na kuongeza;

"Kuna baadhi ya watumishi wa serikali wana ukiritimba mno sasa hizo mbwembwe kafanyeni sehemu nyingine siyo Manyara, haiwezekani mtu eti anajiita mtaalamu wa serikali anafungia kiwanda sababu ya ukosefu wa mlango au kuwa na eneo dogo la kuhifadhi bidhaa," anasema Mnyeti.

Mikakati yao
Mulokozi anasema wanatarajia kufungua kiwanda kingine ambacho kitakuwa cha kuzalisha dawa za binadamu katika eneo hilo hilo la Babati mkoani Manyara na hivi sasa wapo kwenye mchakato wa utafiti kupitia wataalamu waliobobea kwenye fani hiyo waliopo hapa nchini na nje ya nchi.

“Bado kuna changamoto ya urasimu kwa baadhi ya watumishi wa idara za serikali kwani mara nyingi tunapokwenda kwa maofisa wa serikali ili watupatie ushirikiano juu ya unanzishwaji wake inatupa wakati mgumu kwani badala ya kutuambia tupite hapa na pale wenyewe wanakuwa wageni kama sisi kwani hawatambui lolote,” anasema.

Anasema uelewa kwa wataalamu hao bado ni mdogo inatakiwa wazinduliwe kwani ukitegemea upatiwe jibu la hapo hapo inakuwa ni tatizo kutokana na kutakiwa uandike barua kwenye email au njia ya posta badala ya kuwepo kwa dawati maalumu au ofisi ya kushughulikia hilo.

Anasema watumishi hao wanapaswa kuendana na kasi ya Rais John Magufuli ambaye anaelezea sera yake ya Tanzania ya viwanda hivyo wahusika wanapaswa kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha mchakato wake unafanyika kwa haraka na siyo kuzubaisha ili hali hakuna sababu ya ucheleweshwaji.

“Mimi kama mwekezaji nimetafuta mashine na wataalamu sasa mamlaka ya serikali ndiyo inapaswa kuekeleza namna ya kufanya juu ya mchakato wa uanzishwaji wa kiwanda cha dawa na siyo kutuchelewesha yaani unasubiri mwezi mmoja bila sababu badala ya kutekeleza na kuonyesha njia,” anasema Mulokozi.

Anasema wameanzisha kiwanda kingine kupitia kampuni nyingine ya Manyara Breweries iliyosajiliwa miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kufanikisha kiwanda kingine na pia wao ni wakulima wakubwa wa mazao ya mtama, mahindi, maharage na dengu kwenye mashamba yao yalliyopo eneo la Galapo wilayani Babati.

Uboreshaji maslahi ya wafanyakazi wao
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Gasper Mlay anasema kupitia kampuni hiyo, wafanyakazi wao wamepatiwa mtaji wa kuanzisha kikundi cha kuweka na kukopa (Saccos) hivyo kuboresha maslahi ya watumishi ambao kutokana na hali hiyo wanakuwa wanapata muda mzuri wa kupumzika baada ya kutoka kazini

Mlay anasema wana wafanyakazi wengi na wanapokuwa nao lengo siyo kuwaajiri na kuwapa mishahara pekee, pia wanawapa elimu ya malezi ya familia na utawala wa fedha zao, kwani ni taaluma waliyoipata vyuoni ambayo wafanyakazi wengine hawana. 

Anasema wanahakikisha kuwa wanachokipata kinakuwa na tija na pia wanapokuwa na tafrija huwa wanawaalika familia za wafanyakazi wao na wenzi wao ili kuhakikisha upendo, mshikamano na ukaribu unakuwepo kwa familia ikiwemo mahusiano mazuri ya baba, mama na watoto.

“Tukiona sehemu kuna tatizo kuna daktari wa kampuni ambaye yupo na timu yake ataweza kuisaidia familia hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo ushauri nasihi kwa lengo la kuboresha maisha yao na pia kuendelea kufanikisha kampuni,” anasema Mlay.

Historia ya kiwanda
Mulokozi anasema yeye kwa kushirikiana na wenzake wawili ambao awali walikuwa waajiriwa, walisajili kampuni yao Octoba mwaka 2017 na kuanzisha kiwanda hicho kinachozalisha pombe kali za ZEC na Strong katika ujazo tofauti tofauti kwenye kata ya Bagara mjini Babati.

Anasema uwepo wa kiwanda hicho umewanufaisha wananchi wa eneo hilo ikiwemo kutoa ajira kwa mafundi kwani tangu ujenzi wake uanze wametoa ajira za kudumu 31 na ajira za muda mfupi 19 hivyo jumla wana wafanyakazi 50.

“Mafanikio ya hiki kiwanda ni kikubwa kuna hatua tatu ikiwemo ya uwekezaji, ya pili ya kujipima na ya tatu ya kuvuna faida, sisi ni wadau wakubwa wa maendeleo wa eneo hili na pia ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa hapa mkoani Manyara, wafanyakazi wetu wanalipa kodi za nyumba, wanasomesha watoto na wanaishi vizuri,” anasema Mulokozi.

Anasema kupitia Saccos ya kampuni hiyo wafanyakazi wake wanaboresha yao ikiwemo kusomesha watoto na pia wamewapa maagizo ndani ya muda wa miaka mitano wafanyakazi wake wamenunua viwanja na wajenge nyumba kwa lengo la kuboresha maisha yao.
Mkurugenzi wa kampuni ya kiwanda cha pombe kali cha Mati Super Brands Ltd cha mjini Babati mkoani Manyara, David Mulokozi (kushoto) akitoa maelezo kwa viongozi wa mkoa huo walipotembelea kiwanda chake hivi karibuni.
 Wafanyakazi wa kampuni ya kiwanda cha pombe kali cha Mati Super Brands Ltd cha mjini Babati mkoani Manyara, wakiendelea na shughuli za uzalishaji kwenye kiwanda hicho. 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad