HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 26 September 2018

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU KANDA YA TABORA AFANYA ZIARA MAHAKAMA MKOANI KIGOMA

Muonekano wa jengo la Mahakama Kuu, Kanda tarajiwa ya Kigoma lililopo katika ujenzi, Mhe. Jaji Mfawidhi Kanda ya Kigoma alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo linalotarajiwa kukamilika, Juni, 2019.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu,  Kanda ya Tabora (kushoto)  akiongea  jambo na Wakandarasi wa ‘Masasi Construction Company Limited’ wanaojenga jengo la Mahakama Kuu tarajiwa Kigoma.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bw. Moses Mashaka  akimkaribisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Mhe. Salvatory B. Bongole (wa pili kushoto) kabla ya kuongea na Watumishi wa Mahakama mkoani humo (hawapo pichani). Wa pili kulia ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Beda Nyaki na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Flora Mtarania.
Mhe. Jaji Mfawidhi (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo. 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora akipanda mti katika eneo la Mahakama ya Wilaya Kibondo ikiwa ni utekelezaji wa azimio la kuboresha mazingira. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Mhe. Fadhili Mbelwa.

Na Festo Sanga, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kigoma
Jaji Mfawidhi Mahakamu Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Salvatory Bongole amefanya ziara ya kikazi kwa kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama mkoani Kigoma pamoja na ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Mahakama Kuu, Kanda tarajiwa ya Kigoma.
Mhe. Jaji Mfawidhi huyo alifanya ziara yake mkoani humo kuanzia September 17, 2018 hadi September 21, 2018 na alipata fursa ya kukagua Mahakama katika Wilaya za wilaya Kibondo, Kasulu, Kigoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma.
 Akiongea na Watumishi wa Mahakama Mkoani humo hivi karibuni, Mhe. Jaji Bongole aliwaasa  kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
“Kwa yule ambaye atatuhumiwa na kupelekwa Mahakamani na kuthibitika kushiriki katika vitendo vya rushwa, atachukuliwa hatua stahiki za kisheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi” alisisitiza Mhe. Jaji Bongole.
Aidha aliwapongeza  watumishi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwasisitiza kuendelea kuwa na nidhamu kazini pamoja na kufuata maadili ya utumishi wa umma ili kuboresha utendaji kazi wa shughuli za Mahakama kwa umma.
Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi huyo alitembelea na kujionea miradi ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu na Mahakama Kuu, Kanda tarajiwa ya Kigoma inayotarajiwa kukamilika mapema mwaka 2019.
Mbali na ukaguzi wa Mahakama, Mhe. Bongole alipata fursa ya kutembelea Magereza ya Wilaya ya Kasulu, Kibondo na Kigoma  ili kubaini changamoto mbalimbali zilizoko  na kuzitolea ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad