HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 16, 2018

CEO LUHEMEJA NA SIKU 100 NDANI YA DAWASA MPYA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
HII KAZI ITAFANYIKA: Hiyo ni kauli ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati wa utambulisho wake baada ya kuteuliwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa kuwa Afisa mtendaji mkuu wa Mamlaka hiyo.


DAWASA mpya, iliundwa baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kutoa kauli na kutaka DAWASCO na DAWASA ziwe kitu kimoja, agizo ambalo Wizara ya Maji na Umwagiliaji kama wasimamizi wa mamlaka hiyo kuunda DAWASA mpya itakayokuwa na bodi ya wakurugenzi moja. 


Uteuzi wa kwanza wa Rais Dkt Magufuli ni wa Mwenyekiti wa Bodi Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange na baadae kuteuliwa kwa bodi ya wakurugenzi iliyoundwa na wataalamu mbalimbali wa maji.


“Nimshukuru sana Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa kwa uteuzi wake, ameniamini sana kwa kunipa majukumu haya makubwa kuongoza mkoa wa Dar es Saalaam na Pwani,” alianza kwa kusema.

Alisema, Mabadiliko haya ni mabadiliko ya kihistoria, kwa kuona hatua nyingine inapigwa kwa kutatua tatizo la umaskini, malazi na ujinga. Stadi mbalimbali zinaonesha huduma za maji zikiboreshwa kwa asilimia moja uchumi wa nchi huongezeka kwa asilimia nne na huduma zikizorota kwa asilimia moja uchumi hupungua kwa asilimia nne.


Ni kwelil; Kuna changamoto zinazowakabili DAWASA katika suala la upatikanaji wa maji pembezoni mwa mji, Kwa Mkoa wa Dar es Salaam ifikapo mwaka 2030 utakuwa ni moja ya majiji makubwa barani Afrika na ongezeko la watu litakuwa ni Milioni 11 na makadirio ya maji kwa siku yatakuwa ni n Lita Milioni Moja na Laki Moja (1,100,000).


Mhandisi Luhemeja ameweka mikakati mbalimbali ya DAWASA baada ya kukabidhiwa dhamana ya kuiongoza Mamlaka hiyo na hatua ya kwanza ni kuhakikisha miradi iliyokuwa inasuasua inamalizika kwa wakati tena ndani ya siku 100.


Siku 100 za Mhandisi Luhemeja ndani ya DAWASA, mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo ameweza kumuahidi ndani ya siku 100 miradi ya maji iliyokuwa inasuasua na mingine kutokumalizika kwa wakati imepata dawa nayo ni uongozi mpya wa DAWASA.


Mhandisi Luhemeja ameweka wazi , Mradi wa Chalinze tayari wakandarasi wa mradi huo wameshaitwa kujieleza kwenye bodi ,waeleze kwanini mradi huo umekuwa unasuasua kwa kipindi chote na kama tayari wameshatekeleza yale waliyoagizwa na Profesa Mbarawa.


Mradi wa pili ni wa usambazaji maji katika maeneo ya Goba, Salasala, Bunju, Bagamoyo na Kiluvya na mradi huu unatakiwa kukamilika mwisho wa mwezi Oktoba, huku mradi mwingine ukiwa ni Ruvu Juu na Rais Dkt Magufuli aliahidi mradi huo utapeleka maji maeneo ya Kisarawe na tayari serikali imeshalipia malipo ya awali na wapo katika mikakati ya kukamilisha Milioni 700 ili usambazaji huo uanze mara moja.


Mita za malipo ya awali (Prepaid Meter) zilizozinduliwa na Waziri Mbarawa, Mhandisi Luhemeja amesema Kuna changamoto kubwa sana ya madeni na ndani ya siku 100 za DAWASA mpya atahakikisha mita hizo ambazo tayari zimeshaanza kufungwa kufanyika kwa zoezi hilo kwa taasisi zote kubwa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Mita hizi zitaweza kusaidia wizi wa maji unaofanyika na kusababisha hasara kubwa kwa Mamlaka.


Wakati wa uzinduzi wa mita hizi, Profesa Mbarawa aliweka wazi mkakati wa kukomesha wadaiwa sugu ambapo mtumiaji wa maji atatakiwa kulipia maji kabla ya matumizi na hela yake ikimalizika maji nayo yatakatika na pia itasaidia katika kupunguza madeni kwani pindi anapokuja kununua maji atalazimika kulipa kiasi Fulani cha deni.


Mita hizo tayari zimeshafungwa kwenye baadhu ya maeneo ikiwemo viwanda na wateja wa kubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam na Profesa Mbarawa aliagiza hilo zoezi liende kwa kasi sana, na baada ya uteuzi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA mpya ameahidi ndani ya siku 100 wateja wote wakubwa watakuwa wameshafumgiwa mita hizo za malipo ya kabla.

Muelekeo wa DAWASA mpya,Mhandisi Luhemeja amesema kwa sasa wana mikakati ya kupeleka maji Dar es Salaam ya Kusini na ameshakabidhi mradi wa maji wa Kiwalani utakaokuwa na dizaini ya kusambaza maji katika maeneo ya Kitunda, Yombo, Mwanagati, Gongo la Mboto. 


Kumekuwepo pia na malalamiko kuhusu mradi wa Kimbiji na Mpera, utakaozalisha maji Lita Milioni 260 kwa siku ulio chini ya Kampuni ya Serengeti kushindwa kukamilika kwa wakati , Visima vya maji vikiwa tayari vimeshachimbwa kwa asilimia kubwa, Mhandisi Luhemeja ameahidi kupitia upya usanifu wa Matanki yatakayotumika kuweka maji yanayotoka kwenye visima hivyo na matanki hayo ni ya Gongo la Mboto, Chanika, Luanda na Pugu. Luhemeja ameweka wazi kuwa Dawasa kuna wahandisi 12 wenye leseni na mihuri na kwa pamoja Kamati ya wahandisi  wataanza kujenga matanki hayo kwa uwezo wao wa ndani.


Kukamilika kwa matanki hayo kutasaidia upatikanaji wa maji katika maeneo ya Chamazi, Kitunda, Pugu, Ukonga, Kinyerezi na Uwanja wa Ndege. Mradi wa Kimbiji Mpera umekamilika ila umekuwa hauendelezwi ila mpaka kufikia Desemba 9 mwaka huu utakuwa umefikia hatua za mwisho.


Desemba 9 2018 DAWASA mpya inaazimia kutangaza Uhuru wa Maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam , Mhandisi Luhemeja amesema kuwa siku ya uhuru maji miradi mingi itakuwa imekamilika na itakabidhiwa kwa Katibu Mkuu Profesa Mkumbo ikiwemo na kukabidhi ripoti ya mradi wa Benki ya Dunia wa Km 1426 ambao unatarajiwa ifikapo Septemba 15 mkandarasi atakuwa eneo la ujenzi.



Maji Taka, Mhandisi Luhemeja amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya huduma za maji taka toka kwa Mamlaka kutoka na uwekezaji wake kuwa mkubwa ila tayari wameshapanga bajeti kwa kutumia uwezo wa ndani kuwa ifikapo Desemba 9 wawe wanamiliki malori 20 ya kutoa huduma za maji taka kwa wananchi, ila ameainisha changamoto nyingine katika mradi huo ni wamiliki binafsi kujipangia bei na zimekuwa kubwa sana na kuja kwa malori hayo kutasaidia kutoa huduma kwa watanzania kupata huduma kwa bei nafuu.

Ukarabati wa mabwawa, Mhandisi Luhemeja ameweka wazi mkakati wa DAWASA mpya kukarabati mabwawa yote ya maji taka yaliyoharibika na kutengenezwa yaliyopo maeneo ya Mikocheni, Mabibo, Airwing na Buguruni kwa ajili ya kuanza kupokea malori kutoka makazi ya watu.

" Pia tutahakikisha maunganisho ya wateja wa huduma ya uondoshaji maji taka yanaongezekankutoka asilimia n0 ya sasa mpaka kufikia asilimia 40 ifikapo 2020/21,"

Akielezea changamoto ya upotevu wa maji, Mhandisi Luhemeja amesema DAWASA mpya imeacha yale yote yaliyofanywa na DAWASCO, upotevu wa maji umebaki historia, na kwa sasa watahakikisha wanapunguza upotevu mkubwa wa maji na wametenga asilimia 35 ya mapato ya ndani ya kila mwezi kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa usafirishaji maji. Na kuhakikisha ifikapo 2020/21 wakazi wa Dar es Salaam na maeneo yote yanayohudumiwa na DAWASA yanapata huduma ya maji safi na salama kupitia mfumo rasmi kwa asilimia 95.

“Mtandao mdogo wa maji umekuwa unaleta changamoto kubwa katika upotevu wa maji, maji ni mengi yanapokuja kwa wingi yanasababisha kupasuka kwa mabomba na yanapelekea kupotea kwa maji na mapato yatakayotengwa yatasaidia kulaza mabomba na kutatengwa akaunti maalumu kwa ajili ya kuingiza makusanyo hayo ,” amesema Mhandisi Luhemeja.


Tatizo lingine la upotevu wa maji unatokana na mita za maji, kuna mita elfu sitini na nane (68,000) kwa ajili ya kuwafungia wananchi na ili kuhakikisha upotevu wa maji unaondoka, Pia Mhandisi Luhemeja amewaonya wezi wote wa maji kuwa tayari DAWASA mpya imeshasharikiana na kitengo cha Polisi na kuwataka wananchi kushirikiana na Polisi kuwabaini wezi wa maji ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.


Ongezeko la Mapato ndani ya DAWASA mpya, Mikakati iliyopo ni pamoja na kuhakikisha mapato ya ndani yanaongezeka kutoka Bilioni 9.3 mwezi Agosti na kufikia Bilioni 12 na hili litafanikiwa kwa kudhiditi upotevu wa maji kwa asilimia 35 kufikia Desemba ikiwa ni ndani ya siku 100.


Hali ya watumishi ndani ya DAWASA mpya, Mhandisi Luhemeja ameweka wazi kuwa kunzia mwezi ujao mishahara ya wafanyakazi itakuwa na maslahi mazuri yatakayomuwezesha mtumishi maslahi mazuri


Mhandisi Luhemeja ameweka wazi kuwa DAWASA mpya kushindwa sio sehemu yao bali watashirikiana kwa pamoja kuijenga ili ilete manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Malengo hayo ni mikakati madhubuti waliyojiwekea ya kuwa na DAWASA mpya yenye tija na itakayoiinua Wizara ya Maji na Umwagiliaji.


DAWASA mpya rasmi imeanza kazi yake Septemba 9, baada ya kutambuklishwa kwa menejimenti mpya iliyo chini ya Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwa sambamba na Mwenyekiti wa bodi Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange na amewahidi watanzania wote kuwa hususani wa Mkoa wa Dar es Saalaam na Pwani maji yatawafikia sehemu zote chini ya uongozi wake.


Hitimisho, kuundwa kwa DAWASA mpya kunakuja kujena taswira ya mapinduzi ya sekta ya maji iliyokuwa inasuasua kwa kipindi kirefu katik jiji la Dar es Salaam, ili nchi iweze kuinuka kiuchumi haina budi kuwa na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu na hata katika viwanda mbalimbali vikiwemo vya Vinywaji ambao takribani lita laki moja (100,000) zinatumika kwa siku kwenye kiwanda kimoja, ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali nayo imekuwa inatumia maji kwa wingi ili kufanikisha shughuli zao za ujenzi wa maendeleo ya nchi.Napenda kuipongeza Serikali kwa kuunganisha DAWASCO na DAWASA kwa manufaa ya nchi 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumzia siku 100 za Dawasa mpya na mikakati waliyoiweka katika utekelezaji wa miradi ya mamlaka hiyo iliyozinduliwa Septemba 9 mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo. (katikati) akiwa na  Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa bodi ya Dawasa Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange pamoja na Menejimenti mpya  iliyozinduliwa Septemba 9 mwaka.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad