HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 13 August 2018

WAZIRI MKUU AMUAGIZA RPC LINDI KUMKAMATA KATIBU WA TSCWaziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Agosti 12.2018 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Anthon Mandai, akipanda gali la Polisi mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kumuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Pudencis Protas, kumkamata ili akajibu tuhuma zinazomkabili, Agosti 12.2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Ni baada ya walimu kumtuhumu kwa ulevi, rushwa, kughushi nyaraka
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Bibi. Pudencis Protas kumkamata Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wa wilaya ya Ruangwa Bw. Anthon Mandai kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa walimu wakimlalamikia kiongozi huyo kuwa na tabia za kudai rushwa, kutowapandisha madaraja, ulevi pamoja na kuwaita walimu hao kwenye vilabu vya pombe kwa ajili ya kuwasikiliza matatizo yao.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Agosti 12, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa akiwa katika siku ya mwisho ya ziara kyake ya kikazi wilayani hapa. Bw. Mandai anakaimu nafasi hiyo tangu Juni, 2012.

Amesema mbali na kulalamikiwa na walimu kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za ulevi na kuwaita walimu katika vilabu vya pombe pindi wanapohitaji kuhudumiwa, pia amekuwa akighushi nyaraka za mirathi, jambo linalosababisha baadhi ya familia za waliokuwa walimu kuchelewa kupata haki zao.
“Huyu Katibu ameshindwa kuwasaidia walimu katika kutatua changamoto zao na badala yake amekuwa akitumia vibaya majina ya viongozi wakuu, ambapo hata mimi alijaribu kutaka kunichakachua kwa kughushi muhtasari wa kikao cha mirathi ya Mwalimu Suwedi Chikawe akitumia jina langu kuwa nilikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kilichokuwa na agenda ya kumbadilisha msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa na familia jambo ambalo si la kweli,” amesema.

Waziri Mkuu amesema mbali na kukamatwa kwa Bw. Mandai, pia amemuagiza Kamanda Pudencis afanye uchunguzi wa kina utakaowezesha kukamatwa kwa mtandao wa watu wote wanashirikiana na kiongozi huyo katika kughushi nyaraka za vikao vya mirathi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wabadilike na wafanye kazi kwa bidii, waachemazoea na watumie utalaamu wao vizuri katika kuwahudumia wananchi na Serikali haitowavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao.

Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi kuwachukulia hatua watumishi wote wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu wanaitia hasara halmashauri yao na Serikali kwa ujumla.

"Msimamo wa Serikali ni kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo, hivyo watumishi wajiepushe na vitendo vya rushwa na matumizi mbaya ya fedha za umma."
Pia Waziri Mkuu amewataka watendaji hao wawe na mpango wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao hususan ya vijijini kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad