HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 14 August 2018

TAARIFA KWA UMMA: UANACHAMA KATIKA MFUKO WA PSSSF NA NSSF

Mfuko wa PSSSF unaoundwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya PSSSF umeanza rasmi Tarehe 1 Agosti, 2018. Mfuko huu ni mahsusi kwa ajili ya Watumishi wa Sekta ya Umma. Mfuko wa NSSF kwa upande mwingine umekuwa Mfuko mahsusi kwa ajili ya Wafanyakazi katika Sekta Binafsi (Private Sector) na Sekta ya isiyo rasmi (Informal Sector).

Hivyo, kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya PSSSF kikisomwa pamoja na Kifungu cha 6 cha Sheria ya NSSF mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:-
(i) Kuanzia Tarehe 1 Agosti, 2018 waliokuwa Wanachama wa Mifuko iliyounganishwa yaani PPF, PSPF, LAPF na GEPF wamehamishiwa katika Mfuko wa PSSSF na wataendelea kuwa Wanachama na kuchangiwa katika Mfuko wa PSSSF. 

(ii) Wanachama wote wa Mfuko wa NSSF ambao wanatoka (Sekta Binafsi na Sekta ya Umma) wataendelea kuwa wanachama wa Mfuko huo na michango yao itaendelea kuwasilishwa katika Mfuko wa NSSF.

(iii) Watumishi  wapya watakaoajiriwa kuanzia Tarehe 1 Agosti, 2018 katika Utumishi wa Umma, Mashirika ya Umma na makampuni yote ambako Serikali inamiliki zaidi asilimia 30 ya hisa watatakiwa kusajiliwa katika Mfuko wa PSSSF.

(iv) Wafanyakazi watakaoajiriwa katika Sekta Binafsi (Private Sector) au kujiajiri katika Sekta isiyo rasmi (Informal Sector) watasajiliwa katika Mfuko wa NSSF kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na Mfuko wa NSSF.

Tunapenda kuwaondoa wasiwasi Wanachama, Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii na Umma kwa ujumla kuwa huduma zote za Hifadhi ya Jamii zilizokuwa zikitolewa na Mifuko iliyounganishwa zinaendelea kutolewa kama kawaida katika Ofisi zile zile. Endapo utahitaji ufafanuzi zaidi tafadhali msisite kuwasiliana na Mamlaka (SSRA).

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) 
S.L.P 31846
Tovuti: www.ssra.go.tz
DAR ES SALAAM
09/08/2018

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad