HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 10, 2018

KAMPENI YA USAFI KWA FUKWE YAZINDULIWA RASMI LEO JIJINI.

Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii.

Wizara ya Maliasili na Utalii Nchini imezindua  rasmi kampeni ya kufanya usafi katika maeneo ya fukwe kwa ajili ya kuvutia utalii wa fukwe kwa wazawa na wageni iliyoanzishwa na  Bodi ya Utalii nchini (TTB) na Hoteli ya Ramada Resort.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo pamoja na kufanya usafi kwenye Fukwe ya Hotel ya Ramada Resort, Mkurugenzi Msaidizi Leseni na Udhibiti Idara ya Utalii Rosada Msoma amesema kuwa utaratibu huu uliowekwa na Bodi ya Utalii Nchini ya kufanya usafi kutasaidia kuboresha na kuvutia watalii wengi zaidi.

Rosada ambaye ameshiriki kusafisha ufukwe wa Ramada Resort, amesema ana imani kampeni hiyo itakuwa endelevu kwani ni miongoni mwa mipango ya Serikali kuvutia utalii wa fukwe.

"Tutakapokuwa tunafanya usafi kwenye fukwe zetu,  zikiwa safi kiukweli zitavutia utalii na watalii wengi watakuja kutoka sehemu mbalimbali kwa wanaopenda matembezi lakini pia kwa wazawa ni fursa ya kufanya biashara,” amesema Rosada.

Rosada amesema kuwa, wao kama Wizara ya Maliasili zoezi la usafi walilizindua Mwezi April mwaka huu wakiwa na lengo la kuboresha maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya kuvutia watalii nchini.

Mkurugenzi wa masoko wa TTB, Ernest Mwamaja amesema fukwe nyingi hazipo katika hali ya usafi na uchafu wake kwa asilimia kubwa ni makopo ya plastiki yanayoletwa na maji yanayotiririka kutoka kwa wananchi sehemu mbalimbali wanaotupa kwenye vyanzo vya maji kama vile mito.

Mwamwaja amesema kuwa mkakati huu umewekwa madhubuti kwa ajili ya kusafisha fukwe za bahari ya Hindi zilizopo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na leo ikiwa ni uzinduzi rasmi wamedhamiria kufikisha watalii Milioni 2 kwa mwaka ifikapo 2020 ambapo kwa sasa ni watalii 1.3 ndio wanaofika nchini.

"naweza kusema katika suala la usafi kuna haja ya bodi ya utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususani mahoteli kushirikiana kwa pamoja kutoa uelewa kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji ikiwemo na kuwaasa kuacha kutupa taka za plastiki hovyo , madhara yake ni makubwa na lengo letu ni kuongeza utalii kufikia idadi ya watalii milioni mbili kwa mwaka ifikapo 2020,” amesema Mwamaja.

Mwamwaja amesema kuwa wameanza na Hoteli ya Ramada Resort na muitikio ukiwa ni mkubwa na kwa pamoja wameshirikiana na Jeshi la Ulinzi (JWTZ) na Jeshi la Polisi Nchini katika kufanya usafi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa masoko wa Ramada Resort, Bharath Swarup amesema ni jambo jema kuona TTB inawashirikisha wadau katika kampeni kama hiyo ambayo inalenga kutunza mazingira ya fukwe.

“Kupitia fukwe ambazo zimetunzwa vizuri Serikali inaweza kupata mapato ya kodi lakini kama fukwe zimechakaa haziwezi hata kuvutia wageni/watalii,” amesema.

Naye Luteni Kanali JWTZ 43 Kikosi Jeshi Nelson Ponela amesema kuwa tofauti na masuala ya ulinzi wamekuwa wadau wakubwa wa kutunza mazingira wakiwa wanashiriki katika ufanyaji wa usafi wa sehemu mbalimbali na watashirikiana kwa pamoja kulinda mazingira ya fukwe.

Zoezi hili limeweza kushirikiana wakaazi wa Kata ya Mbezi Kutoka serikali ya mtaa ya Kilongawima wakiongozwa na Mwenyekiti wao Paul Richard, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Halmashauri ya Dar es Salaam Gasto Mwakwembe, Kamishna wa Polisi Msaidizi kutoka Makao Makuu Ferdinand Mtui na Afisa utalii Hifadhi za Bahari na Maeneo tengefu Hussein Ngenje.
Wafanyakazi wa Bodi ya Utalii Nchini (TTB) L, Hoteli ya Ramada Resort, Jeshi la Ulinzi, Wananchi wa Mtaa wa Mlongawima wakiwa katikaPicha ya pamoja baada ya kumalizika kwa usafi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Leseni na Udhibiti Idara ya Utalii Rosada Msoma akizungumza na waandishi wa habari  wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kufanya usafi katika fukwe za Bahari kwa ajili ya kuvutia Utalii wa fukwe kwa wazawa na wageni iliyoanzishwa na Bodi ya Utalii Nchini Tanzania (TTB) na Hoteli ya Ramada Resort.
 Meneja Masoko wa Bodi ya Utalii Nchini Tanzania (TTB) Godfrey Meena akiwa sambamba na Kamishna msaidizi wa Polisi Makao Makuu Ferdinand Mtui wakishiriki usafi kafika fukwe za bahari kwa ajili ya kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
 Mkurugenzi wa Masoko wa Hoteli ya Ramada Resort Bharath Swarup akiwa anashiriki usafi  katika uzinduzi wa kampeni ya kufanya usafi katika fukwe za bahari kwa ajili ya kuvutia Utalii wa fukwe kwa wazawa na wageni iliyoanzishwa na Bodi ya Utalii Nchini Tanzania ( TTB) na Hoteli ya Ramada Resort.


Wananchi na wafanyakazi mbalimbali wa Bodi ya Utalii na Hoteli ya Ramada Resort wakiendelea na usafi wakati wa uzinduzi wa kampenk ya kufanya usafi katika fukwe za Bahari kwa ajili ya kuvutia Utalii wa fukwe kwa  wazawa na wageni.

Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii (TTB) Ernest Mwamwaja  (katikatk) akiwa anafanya usafi wakati wa kampeni ya uzinduzi ya kufanya usafu katika fukwe za bahari  kwa ajili ya kuvutia utalii wa fukwe kwa wazawa na wageni iliyoanzishwa na Bodi ya Utalii Nchini Tanzania (TTB) na Hoteli ya Ramada Resort. Picha ya chini akiwa anazungumza na wanahabari baada ya kumaliza usafi.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad