HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 3 July 2018

MECHI 16 BORA ZA SPRITE BBALL KINGS KUPIGWA JUMAMOSI NA JUMAPILI

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
Droo ya hatua ya 16 bora ya michuano ya Sprite BBall Kings imefanyika jana usiku moja kwa moja na kila timu kumfahamu mpinzani wake ikishuhudiwa na viongozi wa Shirishiko la Mpira wa Kikapu Nchini.

Timu 16 zilifanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kucheza mechi za mchujo mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya JMK Youth Park zikiwa timu 50 kutoka sehemu tofauti za Jijini Dar es Salaam.

Manahodha wa timu zilizofanikiwa kuingia hatua ya 16 bora wamejitapa kuondoka na ushindi  kila mmoja akimtaka mpinzani wake ajipange.

Kwa upande wa Nahodha wa timu ya Mchenga BBall Stars Mohamed Yusuph ambaye timu yake itapambana na Oysterbay amesema kuwa hiyo ni mechi nzuri na itakayokuwa na ushindani mkubwa sana.

Nahodha wa Portlands Denis Babu akishika nafasi ya pili ya ufungaji akiwa na Pointi 19 amesema kuwa mechi yake dhidi ya Mbezi Beach KKKT itakuwa ni mechi ngumu sana kwani hawafahamu vizuri  na hata wachezaji wake wengi hajawafahamu ila anaamini ushindani utakuwa ni mkubwa.

Manahodha mbalimbali walitambiana huku wengine wakiweka wazi kuwa hawakuwa tayari kukutana na bingwa mtetezi Mchenga BBall Stars kwani wanaamini safari yao ya kwenda hatua ya nane bora ingekuwa ngumu sana.

Mechu nne za kwanza zitachezwa siku ya Jumamosi katika Viwanja vya Air Wing Ukonga ikizikutanisha timu za Fast Heat dhidi ya DMI, Flying Dribblers na Ukonga Heatmen, St Joseph dhidi ya Airwing pamoja na Mbezi Beach KKKT akichuana na Portland.

Siku ya Jumapili mechi zingine nne zitachezwa kwenye Viwanja vya Bandari Kurasini zikiwakutanisha Mchenga BBall Stars dhidi ya Oysterbay, Stylers akipambana na Temeke Heroes, Mechi nyingine ni Ukonga Warriors dhidi ya The Team Kiza na mchezo wa mwisho utakuwa ni mpambano baina ya Raptors akichuana na Water Institute.

Michuano ya Sprite BBall Kings 2018 yanayodhamiwa na kinywaji cha Sprite yameanza mwishoni mwa wiki kwa hatua ya mchujo kufanyika, timu 16 kufanikiwa kuvuka na zinaenda kukutana siku ya Jumamosi.

Mshindi wa kwanza atafanikiwa kuondoka na kitita cha Milioni 10 pamoja na Kombe, Mshindi wa pili milioni 3 na mchezaji bora wa mashindano  akitwaa milioni 2 .


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad