HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 11 July 2018

Balozi wa Korea, Dk Mengi wazungumzia uunganishaji magari ya Korea nchini Tanzania


BALOZI wa Korea Kusini, Mh. Geum-Young Song amesema kwamba  atasaidia haja ya uwekezaji wa uunganishaji magari nchini Tanzania pamoja na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha tehama kwa nchi za Kusini, Kati na Mashariki ya Afrika.
Alisema hayo kwenye mazungumzo na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Ltd, Dk. Reginald Mengi ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Katika mazungumzo hayo Balozi huyo wa Korea Kusini alisema kwamba atahakikisha anafanya kila kinachowezekana kushawishi makampuni ya magari ya Korea kusini kuanza kuunganisha magari hayo nchini Tanzania.
Dk. Mengi katika mazungumzo hayo alisisitiza haja ya kuanza mazungumzo ya kina ya ushirikiano katika kuunganisha magari kabla ya kuingia katika masuala ya simu zenye utendaji wa kisasa (Smart Phones) na tehama kwa ujumla.
Alisema pamoja na kukubaliana na wazo la Dk. Mengi kuhusu haja ya kuwa na kampuni ya kuunganisha magari nchini Tanzania katika kuelekea uchumi wa viwanda taifa kutengeneza magari yake yenyewe, alisema kama taifa wana mpango wa kusaidia Tanzania kuwa taifa la viwanda likiongoza katika tehama.
Alisema kwa kuwa taarifa na mambo mengi ya habari ndio nguvu kwa vijana kuelekea katika ustawi wangelipenda kuwa na  eneo ambalo vijana watalitumia katika kupata maarifa na kuyatumia kuboresha hali zao na kukua kiuchumi.
Katika mazungumzo hayo Dk. Mengi alisema kwamba kuwapo na viwanda vya magari nchini Tanzania ni ndoto yake na kwamba alikuwa amepanga kwenda Sri Lanka kushawishi ushirika katika uunganishaji magari kuelekea kuyatengeneza Tanzania.
Alisema kutokana na mazungumzo na balozi huyo, ataahirisha ziara yake na kuzungumza na makampuni ya Korea kwa kuwa tayari bidhaa za nchi hiyo zikiwemo magari ya Kia na Hyundai yana soko nchini na itakuwa jambo la heri kuunganisha magari hayo nchini.
Alisema kwamba kama watakubaliana kuanzisha uunganishaji wa magari anaamini hatua itakayofuata ni kutengeneza gari hilo kwani nia yake ni kuhakikisha kwamba gari hilo baada ya miaka michache linatengenezwa lote kwa mali ghafi za Tanzania na hivyo kutanua zaidi ajira.
Alisema kwamba Korea Kusini miaka michache baada ya uhuru wa Tanganyika, ilikuwa sawa na  Tanganyika, lakini hapa katikati walitumia vyema fursa zilizokuwepo kusonga mbele na kwa sasa taifa la Tanzania nalo linataka kujikita katika viwanda na kuna fursa kubwa ya uwekezaji na soko la uhakika.
Dk. Mengi alitaka kasi katika kukamilisha mazungumzo kuhusu suala hilo la kuunganisha magari ya Hyundai na Kia nchini na kwamba anataka kushiriki katika mradi huo.
Balozi huyo alisema kwamba atahakikisha kwamba anafanyakazi ya kuunganisha makampuni ya Korea na wawekezaji wa Tanzania kwa lengo la kuhakikisha kwamba wanakuza diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Korea Kusini.
Alisema kwamba tangu kuanzishwa kwa ushirikiano wa kibalozi mwaka 1992 uhusiano wa mataifa haya mawili umeendelea kukua katika nyanja mbalimbali za ushirikiano.
Alisema anaamni kwamba Tanzania itapiga hatua kubwa kiuchumi chini ya usimamizi wa uhakika wa serikali ya awamu tano chini ya Rais Dk John Magufuli.
Alisema mchango wa Korea Kusini ni kuendelea kufanya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na kubadilisha uzoefu kupitia programu yake ya Knowledge Sharing Program (KSP) yenye kutoa fursa ya mataifa mengine kujifunza kutoka Korea Kusini. 
Alisema kwamba Tanzania imeteuliwa kama mshirika wa uhakika wa kupatiwa misaada kupitia Official Development Assistance (ODA) kuanzia mwaka 2016 na hivyo ipo tayari kuishirikiana na Tanzania katika masuala ambayo yana maslahi kwa pande zote mbili.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Ltd, Dk. Reginald Mengi akizungumza na Balozi wa Korea Kusini nchini, Geum-Young Song wakati Balozi huyo alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Biashara na Uwekezaji wa Korea, Hong Kyun Lee. Balozi wa Korea, Dk Mengi wazungumzia uunganishaji magari ya Korea nchini Tanzania

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad