HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 5 June 2018

UONGOZI SHULE YA ST FLORENCE WAMZUNGUMZIA MWALIMU ANAYETUHUMIWA KWA KUDHALILISHA WANAFUNZI WA KIKE

Na Ripota Wetu, Globu ya Jamii

UONGOZI wa Shule ya St Florence Academy ya jijini Dar es Salaam umesema umesikitishwa na habari za mmoja wa walimu wake kutuhumiwa kuwadhalilisha wanafunzi wa kike kijinsia huku ikifafanua kuwa umejipanga kuongeza CCTV Camera katika sehemu mbalimbali za shule ili kuimarisha usalama

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Shule hiyo, Flora Damas Assey amesema kuwa wao kama uongozi, wazazi na walezi wamesikitishwa mno na taarifa hizo.

"Hii ndio mara ya kwanza mwalimu wa shule yetu ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka 25 iliyopita kupatwa na tuhuma kama hizi na tumekuwa tukijitahidi kuajiri walimu makini na kujenga imani kwa wazazi na jamii nzima kwa ujumla kutokana na matokeo mazuri ya wanafunzi wetu na nidhamu ya hali ya juu ambayo inaendana na sera ya shule yetu,"amesema Assey.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uongozi wa shule hiyo umetoa ushirikiano mkubwa kwa Jeshi la Polisi ambalo linachunguza suala hilo na tayari uongozi na kamati ya shule umekutana na kukubaliana kutekeleza masuala kadhaa.

"Tunapenda kukanusha taarifa zilizozagaa hivi karibuni kuwa shule imemficha mwalimu huyu anayetuhumiwa kwani hata sisi hatujui aliko na tunaendelea kushirikiana na Polisi katika suala hili,"amesema huku akitoa mwito kwa wananchi pia walisaidie Jeshi la polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

Mkurugenzi huyo amesema baadhi ya mambo walioazimia kufanya ni kuongeza CCTV camera katika sehemu mbalimbali za shule ili kuimarisha usalama,  kuimarisha uchunguzi wa ndani mara kwa mara na kuimarisha kitengo cha ushauri ili wanafunzi wapate usimamizi wa karibu na waendelee kupata ushauri  (counseling) pale inapohitajika.

"Kama uongozi wa Shule ya St. Florence tunatoa rai kwa wazazi wote wawe na subira wakati huu ambao polisi wanaendelea na uchunguzi na shule itatoa ripoti mara kwa mara kuhusu suala hili,"amesema.

Pia amesema shule inaendelea na maandalizi ya mtihani wa darasa la saba na kuwataka wazazi na walimu washirikiane na uongozi kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana.

"Tumekuwa tukifanya vizuri katika mitihani mbalimbali inayosimamiwa na Baraza la Mitihani Tanzania na kupokea vyeti na tuzo mbalimbali kutoka serekalini na taasisi mbalimbali kutokana na matokeo haya ambayo tuko tayari kuhakikisha tunayaendeleza,"amefafanua na kuongeza St.Florence Academy, ambayo ni moja ya shule bora nchini, ilianzishwa  mwaka 1993.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad