HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 5, 2018

AAR YAPANDA MITI SHULENI KUSAIDIA UTUNZAJI BORA WA MAZINGIRA

Kampuni ya bima ya afya nchini ya AAR imepanda miti katika Shule ya Msingi ya Ushindi iliyoko eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono kwa vitendo utunzaji wa mazingira.

AAR imefanya zoezi hilo Jumanne wiki hii ikipanda jumla ya miti sitini (60) katika shule hiyo ya umma iliyo kwenye eneo lililo karibu na ofisi zake za makao makuu, katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani.

Akizungumza baada ya upandaji miti, Msemaji wa AAR, Hamida Rashid amesema kuwa kuboresha na kulinda afya ya jamii ni sehemu muhimu ya jukumu la kampuni hiyo, hivyo haina budi kusaidia na kuhamasisha kwa vitendo utunzaji wa mazingira katika jamii inayoizunguka kwani ndio msingi wa uhai.

“Tunafamu mazingira ni muhimu katika maisha yetu kwani ubora wa afya na uhai wetu unategemea hali ya mazingira yetu.  Kama kampuni ya bima ya afya ambayo hujikita katika kuboresha na kulinda afya ya jamii, tunaamini kwamba ni jambo lisilowezekana kuwa na jamii yenye afya bora bila kuhakikisha kuwa jamii inaishi kwenye mazingira bora yanayohifadhiwa vizuri,” alisema Hamida 

“Ndio sababu tumeamua kuhamasisha jamii kwa vitendo kupanda miti. Tunaamini elimu ya mazingira ikitolewa vizuri kwa jamii kuanzia kwa watoto shuleni tutajenga taifa la wachapakazi ambalo ni rafiki wa mazingira,” Hamida aliongeza.  

Aidha, Hamida alitoa wito kwa makampuni mengine pamoja na watu binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali kulinda mazingira ili kuhuisha ukuaji wa taifa lenye afya bora. Pia, aliwataka walimu kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya mazingira kwa kutenda.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ushindi, Elias Erick Katunzi aliwashukuru AAR kwa kujitolea kuboresha mazingira ya shule hiyo na kuahidi kuendelea kuwafundisha wanafunzi kuwa rafiki wa mazingira. 

“Tunawashukuru AAR kwa kutuhamasisha kwa vitendo na kuboresha mazingira yetu. Kwakuwa tunafahamu mazingira yako katika hatari kubwa kutokana na shughuli mbalimbali na matendo ya binadamu, tunauthamini sana mchango huu. Tunaahidi kuitunza vizuri miti hii na kuhakikisha utunzaji wa mazingira unakuwa tabia endelevu,” alisema Mwalimu Katunzi na kutoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano wa AAR ili kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha nchi inakuwa na mazingira salama na yenye afya nzuri.

Upandaji miti huo umefanyika ikiwa ni wiki moja baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, January Makamba kutoa wito kwa taasisi na watu binafsi kuunga mkono kwa vitendo kampeni za kutoa elimu na uelewa kwa jamii katika ngazi zote.

Ripoti mbalimbali za Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa zimekuwa zikitahadharisha kuhusu hatari ya sehemu ya dunia kugeuka jangwa kutokana na ukataji miti uliokithiri na kutopanda miti; na kuhimiza upandaji miti kama hatua ya utatuzi.
 Meneja wa Maendeleo na Biashara wa AAR Insurance, Hamida Rashidi (kulia) akishiriki katika zoezi la kupanda miti lililoandaliwa na Kampuni ya Bima ya AAR katika siku ya kusheherekea siku ya mazingira duniani
 Wafanyakazi wa AAR Insurance, Sammuel Budodi (kushoto) na Geophray Peter(katikati) wakipanda mti pamoja na mwanafunzi wa shule ya msingi ya Ushindi katika siku ya Mazingira Duniani
Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ushindi Mikocheni wakipanda Miti katika zoezi liloandaliwa na Kampuni ya Bima ya AAR ikiwa ni ishara ya kusherekea siku ya Mazingira Duniani
 Wafanyakazi wa AAR Insurance wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ushindi Mikochi mara baada ya kumaliza zoezi la kupanda miti  ikiwa ni ishara ya kusherekea siku ya Mazingira Duniani.
 Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ushindi, Mikocheni wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumaliza zoezi la kupanda Miti lililoandaliwa na Kampuni ya Bima ya AAR ikiwa ni ishara ya kusherekea siku ya Mazingira Duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad