HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 29, 2018

Tigo yatoa ofa murwa kwa simu janja za kisasa zenye vifurushi vya intaneti katika maonesho ya sabasaba

Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo alipotangaza kuwa kwa mwaka wa tatu mfululizo, Tigo ndio mdhamini mkuu wa mawasiliano katika Maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Dar es Salaam ya Biashara (DITF) ambayo yanaandaliwa na Mamlaka ya Ukuzaji wa Biashara Tanzania (Tantrade). Kushoto ni Meneja wa Ukuzaji wa Biashara wa Tantrade, Stephen Koberou.

Kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali ya Tigo ndio mdhamini mkuu wa mawasiliano katika Maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Dar es Salaam ya Biashara (DITF) ambayo yanaandaliwa na Mamlaka ya Ukuzaji wa Biashara Tanzania (Tantrade). Kauli mbiu ya maonesho hayo almaarufu Sabasaba yanayofanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2018 ni ‘Ukuzaji wa Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda’.

Akitambulisha udhamini huo jijini Dar es Salaam leo, Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kuwa hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Tigo kudhamini maonesho hayo. Ushirikiano huu ni sehemu mojawapo ya azma ya Tigo kuchangia juhudi za serikali kukuza biashara kama njia mojawapo ya kukuza uchumi wa viwanda nchini.

‘Tigo inatambua kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi za Afrika ambapo uchumi wake unakua kwa kasi ya juu na kuwa bado kuna fursa nyingi zinazopatikana nchini. Kila mwaka kwa kipindi cha miaka 42 sasa, Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam ya Biashara (DITF) yamekuwa chachu kubwa ya kukuza uchumi wa viwanda kwani yanatoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wa kati kuonesha ubunifu katika bidhaa na huduma, pamoja na teknologia mpya kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Vilevile, Sabasaba ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwani inatoa fursa za ajira na mapato kwa sekta tofauti,’ Woinde alisema.

Aliwahamasisha Watanzania kujiandaa kupokea ofa kabambe za simu janja za kisasa zenye ofa murua za vifurushi vya intaneti kwa kipindi cha hadi miezi sita kutoka Tigo. ‘Tumeingia ubia na watengenezaji wakubwa wa simu duniani kama vile Tecno, Samsung, Nokia na Freetel kuhakikisha kuwa wateja na wananchi watakaofika katika viwanja vya Sabasaba, Dar es salaam au katika maduka yote ya Tigo nchi nzima wanafaidika na simu janja kwa bei nafuu kuanzia TSH 69,000 pekee katika msimu huu wa Sabasaba.’

Kwa upande wake, Meneja wa Ukuzaji wa Biashara wa Tantrade, Stephen Koberou aliwashukuru Tigo kwa kuchukua jukumu la kuthamini maonesho ya mwaka huu ya Sabasaba ili kukuza biashara. Pia aliwahamasisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi ili waweze kujionea ubunifu na teknologia mpya, kujifunza, kujenga mahusiano mapya ya kibiashara pamoja na kuwa sehemu ya fursa kubwa zaidi ya kufanya manunuzi na kupata huduma muhimu kwa bei nafuu.

‘Maandalizi yako tayari na nawakaribisha wafanyabiashara wote kujitokeza kwa wingi kuunga mkono wafanyabiashara wenzao wa ndani na nje ya nchi ambao wameleta bidhaa na huduma zao katika maonesho ya mwaka huu, huku wakipata fursa ya kujionea hatua kubwa tulizopiga katika kukuza uchumi wa viwanda nchini,’ alisema.

Sabasaba imejizolea umaarufu kama maonesho yanayoongoza nchini kwa kuvutia mamia ya wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na maelfu ya wageni wanaovutiwa na bidhaa bora na bei nafuu zinazopatikana katika maeonesho hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad