HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 14, 2018

AAR YAANDAA FUTARI KWA KIKUNDI CHA TUSHIKAME NA KUTOA MSAADA WA VITANDA

Kampuni ya Bima ya Afya ya AAR imewafuturisha wazee wanaotunzwa katika ‘Kituo cha TUSHIKAMANE PAMOJA cha jijini Dar es Salam na kuwapa msaada wa vitanda kama sehemu ya mchango wao katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mkuu wa Itifaki wa BAKWATA, Shekh Mohammed Nassor akiambatana na viongozi wengine wa kidini waliongoza futari hiyo, iliyofanyika jana jioni, Juni 13, 2018 katika Ofisi za Makao Makuu ya AAR yaliyoko Mikocheni jijini Dar.

Akizungumza katika hafl hiyo, Shekh Mohamed ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi, aliwapongeza AAR kwa kuwajali watu wenye uhitaji hususan wazee ambao alisema wanahitaji uangalizi maalum na faraja. 

Aidha, aliitaka jamii kwa ujumla kushiriki katika kutatua matatizo yanayowakabili wazee, akifafanua kuwa hata Mtume Muhammad (S.W.A) alionesha mfano katika hili akieleza kuwa, “Kama kijana atamheshimu mzee wakati wa umri wake, Mwenyezi Mungu atamteulia mtu atayemheshimu na kumjali wakati wa uzee wake pia.”

“Tunapotumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kutafakari afya za roho zetu, tunapaswa kuhakikisha mazingira ya upendo na kuwajali wenye mahitaji maalum na hata wapita njia. Ninawapongeza AAR kwa kujali hali za wazee ambao ni kisima cha busara ambazo kama taifa tunaweza kuzitumia kuepuka migogoro isiyo ya lazima,” alisema Shekhe Mohammed.

Alitoa wito kwa Waislam nchini kuimarisha imani yao katika kumtii Mwenyezi Mungu na kumuombea Rais John Magufuli pamoja na viongozi wengine wa Serikali ili waendelee kuliongoza taifa kwa amani; na kwamba amani, utulivu na maelewano havina budi kudumishwa ili jitihada za dhati zinafanyika za kuleta maendeleo zaidi ziweze kufanikiwa.

Mapema, Meneja Mkuu wa Kampuni ya AAR, Bi.Violet Modichai aliwashukuru Viongozi hao wa BAKWATA kwa kukubali mwaliko wa kushiriki tukio hilo, hatua ambayo alisema imelibariki na kuwafariji wazee kwa kufuturu nao pamoja. 

Alisema kuwa kampuni hiyo ya bima ya afya inajali kwa kiwango cha hali ya juu kuhusu hali ya wazee kama ilivyo kwa makundi mengine katika jamii kwa ujumla na kwamba hiyo ndiyo sababu iliyowafanya kuandaa futari hiyo kuonesha upendo, kujali na faraja kwa wazee.

Bi. Modichai alisema kuwa pamoja na kuandaa futari hiyo, kampuni hiyo imekichangia kituo hicho cha kuwatunza wazee vitanda kwani wazee hao wanapaswa kuwa na sehemu nzuri ya kupumzika na kupata usingizi mzuri hali ambayo ni muhimu kwa afya yao.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa kujitoa kwetu katika kuboresha hali ya afya ya jamii na kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya afya bila kujali umri wake, ni kwa uhakika na endelevu,” alisema Bi. Violet baada ya kukabidhi vitanda hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya wazee hao, Mwenyekiti wa Tushikame Group, Bi Rose Mwapachu aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwajali na kuwaandalia futari hiyo na kutoa wito kwa makampuni mengine pamoja na watu binafsi kuchukua hatua kwa vitendo katika kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili wazee.
 Mkuu wa Itifaki wa BAKWATA, Shekh Mohammed Nassor akizungumza na Wazee wa Kikundi cha Tushikame Pamoja kilichohudhuria Futari iliyoandaliwa na Kampuni ya Bima ya AAR.
  Mwenyekiti wa Kikundi cha Tushikame, Bi. Rose Mwapachu akitoa shukrani kwa Uongozi wa Kampuni ya AAR kwa kuwakaribisha Futari hiyo pamoja nakusaidia baadhi ya vitu kama Vitanda.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya AAR, Bi. Violet Modichai akikabidhi baadhi ya vifaa kwa Wazee hao wa Kikundi cha Tushikame kilichopo Kwembe.
Sehemu ya Wazee wa Tushikame Group waliohudhuria Futari iliyoandaliwa na Kampuni ya AAR kwenye Makao Makuu yaliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad