HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 25 May 2018

TMRC YAZINDUA MPANGO WA HATIFUNGANI WA MIAKA MITANO WENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 120

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
KAMPUNI ya Utoaji Mikopo kwa Mabenki na Taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC), imezindua mpango wa hatifungani wa miaka mitano kwenye Soko la Hisa (DSE).

Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo Ammish Owusu-Amoah ameongoza uzinduzi huo ambao pia umeshuhudiwa na wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali toka sekta za fedha, nyumba na sekta nyingine.

Hivyo uzinduzi wa utoaji wa dhamana ya TMRC ulifanyika baada ya TMRC kupokea kibali kwa ajili programu ya utoaji wa dhamana ya miaka 5 yenye thamani ya Sh. Bilioni 120. Mpango huo ulipata kibali kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (CMSA) pamoja na Soko la Hisa (DSE). Kampuni hiyo ya TMRC itaorodheshwa kwenye DSE.

Aidha, CMSA na DSE, zilijumuisha kuendelea kwa TMRC kutoa dhamana ya ushirika wake ambayo itakuwa kiasi cha Sh Bilioni 12.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya amesema wamepokea vibali vyote muhimu na tunatarajia kwenda kwenye Soko la Hisa kwa mara ya kwanza hivi karibuni na kufafanua TMRC ni taasisi maalum ya sekta binafsi ya Fedha ambayo hutoa fedha za muda mrefu kwa taasisi za fedha kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba.

Ameongeza taasisi hiyo ina lengo la kuunga mkono taasisi za kifedha kutoa mikopo ya nyumbaya muda mrefu ambayo husaidia kushusha marejesho ya kila mwezi na kuwezesha wateja wengi kumudu.

"Aina hii ya kukopesha pia inajulikana kama mikopo ya jumla.TMRC inatafuta fedha ili kusaidia shughuli zake za mikopo ya nyumba. "Ilifikiriwa tangu mwanzo kwamba TMRC itapata fedha kutoka kwenye masoko ya mitaji kupitia utoaji wa dhamana kati ya vyanzo vingine,"amesema Mgaya na kuongeza "Ilikuwa tu suala la muda na sasa ni wakati mzuri kwa sababu riba za soko zimekua zikishuka."

Pia ametumia nafasi hiyo kuhimiza wenye taasisi za fedha kujitokeza kwa wingi katika hatifungani hizo kwa ajili ya kupata mikopo ya ujenzi wa nyumba na kufafanua unafuu wa riba uliopo sasa utakuwa chachu ya wao kufanikisha ndoto yao ya kuona watanzania wengi wanakuwa na nyumba ambazo wazinunua kwa kulipa kidogo kidgo badala ya kuendelea kupanga kwa gharama kubwa.

"Lengo letu ni kuona wenye benki wanajitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hii na wiki ijayo tunaanza kwa kutoa hatifungani yenye thamani ya Sh.bilioni 12 na kisha tutaendelea kuzitoa kadri tunavyoweza.Pia tumeanza na hatifungani ya miaka mitano lakini huko mbele tutaongeza muda ikiwezekana iwe miaka saba au 10,"amesema Mgaya.

Amesema kuwa hadi sasa wametoa mikopo 26 kwa mabenki 16 huku akisisitiza ni wataendelea kutoa mikopo kwa mabenki lakini watakuwa wakifuatilia vigezo ambavyo wameweka kwa lengo la kuleta tija.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Utoaji Mikopo kwa Benki na Taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC) Oscar Mgaya akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB Plc, Ineke Bussemaker( wa tatu kutoka kulia) pamoja na Mwenyekiti wa TMRC ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya BOA Tanzania, Ammishaddai Owusu-Amoah, wakikata kwa pamoja utepe wa uzinduzi wa mpango wa hatifungan.
 Mtendaji Mkuu wa Fedha wa TMRC, Oswald Urassa akiwaelezwa wadau mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa kampuni ya TMRC.
 Mwenyekiti wa kampuni ya TMRC, Ammishaddai Owusu-Amoah, akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa mpango wa hatifungani wa miaka mitano kwenye Soko la Hisa (DSE).
Baadhi ya wageni walioshiriki wakimsikiliza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Utoaji Mikopo kwa Benki na Taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC) Oscar Mgaya  kwenye uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad