HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 7 May 2018

Taasisi za Fedha Zakopesha Shilingi Bil. 59.2 kwa Wananchi Kupitia Hati za Kimila

Na: Frank Mvungi - MAELEZO, Dodoma
Serikali imesema kuwa Bilioni 59.2 zimekopeshwa na Taasisi za Fedha kwa wananchi kupitia hati za kimila katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akijibu swali  la Mheshimiwa Venance Mwamoto mbunge wa Kilolo (CCM) leo Bungeni, Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Anjelina Mabula amesema kuwa wananchi wameweza kutumia hati za kimila kujipatia mikopo kutoka Benki mbalimbali ikiwemo NMB PLC, CRDB PLC, Stanbic Bank, SIDO na PSPF.
"Natoa rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika miradi ya utoaji wa Hati za Kimila inayotekelezwa katika maeneo yao ili ziweze kuwanufaisha kwa ustawi wa kiuchumi na kijamii," alisisitiza Mhe. Mabula
Akifafanua Mhe. Mabula amesema kuwa kufikia mwezi Machi, 2018 jumla ya hatimiliki za kimila 56,506 zimeandaliwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo wananchi katika maeneo hayo wamenufaika kiuchumi kutokana na mikopo waliyopata kutoka taasisi za kifedha.
Aliongeza kuwa kuna faida nyingi za Hati ya Kimila ikiwemo usalama wa milki, kupunguza migogoro baina ya watumiaji wa  ardhi, kutumika kama dhamana katika taasisi za fedha na vyombo vya kisheria.
Aidha Mhe. Mabula alitoa rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika miradi ya utoaji wa hati za hakimiliki za kimila inayotekelezwa katika maeneo yao ili ziweze kuwanufaisha kwa ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa fungu la 18, 22 hadi 47 la sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999, hati ya hakimiliki ya kimila ardhi kwa kuzingatia mila na desturi kwa raia wa Tanzania na ina hadhi sawa na hakimiliki nyingine inayotolewa kisheria.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Anjelina Mabula akieleza juu ya faida za hati za kimila ikiwemo  kutumika kuwapatia mikopo wananchi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad