HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 7 May 2018

Leseni za madini kuanza kutolewa muda wowote

Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa zoezi la utoaji wa leseni kwa ajili ya utafiti, uchimbaji na biashara ya madini linatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa mara baada ya uanzishwaji wa Tume ya Madini.
Profesa Msanjila ameyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari  kwenye mkutano wa baraza la kwanza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro  tarehe 07 Mei, 2018 wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya zoezi hilo, Profesa Msanjila amesema kinachofanyika kwa sasa ni uchambuzi wa maombi ya leseni zote zilizokwishawasilishwa na kampuni mbalimbali zenye lengo la kujihusisha na shughuli za madini nchini.
Katika  hatua nyingine, akielezea mkutano huo, Profesa Msanjila amesema mkutano huo wa kwanza unaambatana na uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi ambalo lipo kisheria.
Ameendelea kueleza kuwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa umma.
Ametaja masuala mengine kuwa ni pamoja na mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amesema kuwa tayari tume imekaa na kuweka mkakati  kuhusu masuala ya leseni ili kuhakikisha kuwa leseni zinatolewa kwa wakati baada ya zoezi la utoaji wa leseni kusitishwa tangu Julai mwaka 2017.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya zoezi la uchambuzi wa leseni, Profesa Kikula amesema zaidi ya leseni 8,000 zimeshachambuliwa na kusisitiza kuwa zoezi litakapokamilika  waombaji waliokidhi vigezo watataarifiwa ili kuanza kufanya taratibu za malipo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William amesema kuwa baraza la wafanyakazi ni chombo  muhimu kinachowaunganisha wafanyakazi wa Wizara katika uongozi kwa pamoja mahali pa kazi ili kuleta tija katika utekelezaji wa shughuli za Wizara.
Amesema baraza huishauri Wizara juu ya kuongeza ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na Wizara ni za kuridhisha kulingana na malengo ya Taifa ya kuleta maendeleo na kupunguza umaskini kwa kuanzisha viwanda vingi vitakavyoongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi wa Taifa.
Ameendelea kusema kuwa baraza hilo hujadili na kushauri mipango na bajeti ya wizara na kupima mafanikio na kuridhia utekelezaji wake pamoja na upandishwaji wa vyeo wafanyakazi kutokana na miundo ya utumishi.
 Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.
 Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akitoa ufafanuzi katika mkutano huo
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa nne kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad