HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 25 May 2018

Mkuu wa Mkoa Mwanza akagua maghala ya ununuzi wa pamba

 Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Mkuu wa Mkoa Mwanza John Mongella amewataka viongozi na watendaji mbalimbali wakiwemo wa vyama vya msingi vya ushirika AMCOS kuwahamasisha wakulima kuongeza kasi ya uvunaji wa zao hilo ili kunufaika na msimu mpya wa ununuzi ambao tayari umeanza.

Mongella ametoa rai hiyo hii leo baada ya kufanya ziara wilayani Misungwi ili kujionea hali ya ununuzi wa pamba baada ya msimu mpya kuzinduliwa Mei Mosi mwaka huu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Kijiji cha Bukama wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo ya kutembelea maghala mbalimbali ya vyama vya msingi vya ushirika AMCOS wilayani Misungwi, Mongella amewataka wasimamizi wa zoezi hilo kuhakikisha mizani haichezewi kwa minajili ya kuwapunja wakulima.

Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi Bodi ya Pamba Tanzania, James Shimbe amesema tayari bodi hiyo imetoa leseni za ununuzi wa zao la pamba kwa vyama vya msingi vya ushirika AMCOS ambapo amewataka wanunuzi wote kuhakikisha wanachukua leseni hizo ili kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Naye John Masalu ambaye ni Meneja Shughuli, Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza amesema maandalizi yote yamekamilika hivyo ni wakati mwafaka wakulima kunufaika na zao la pamba kupitia AMCOS ambazo zinasimamia zoezi hilo.

Issa Malando ambaye ni mwandishi AMCOS ya Mwalu Mabuki amesema bei ya pamba hivi sasa ni shilingi 1,100 kwa kilo moja hivyo matarajio ni wakulima kuanza kuuza pamba kwa wingi licha ya kwamba baadhi yao bado wanaendelea kuvuna.

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Mkuu wa wilaya Misungwi, Katibu Tawala wilaya hiyo Peter Michale amesema zaidi ya vituo 100 vya ununuzi wa pamba vimejiandaa vyema kusimamia zoezi hilo ambapo tayari vituo 18 vimepokea zaidi ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya malipo ya wakulima.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad