HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 3 May 2018

LAZIMA TUSIMAMIE NIDHAMU, HATA AKIKOSEA MWALIMU AMBAYE NI MKE WA KIGOGO ACHUKULIWE HATUA-KATIBU TUME YA UTUMISHI WA WALIMU

*Apiga marufuku mwanafunzi kuchapwa viboko shuleni, atoa mbinu za ufundishaji
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
KATIBU wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania Winfrida Rutahinfwa ametoa  maagizo kwa Walimu wakuu na Wakuu wa shule nchini kutoogopa kuwachukulia walimu ambao watabainika wanakiuka nidhamu ya utumishi hata kama walimu hao watakuwa ni wake wa viongozi wa ngazi za juu Serikali.

Pia amewaagiza walimu kubuni mbinu za kufundisha wanafunzi ili wafaulu kwenye masomo huku kwa walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam hasa wa Shule za Sekondari kujikita katika kufundisha wanafunzi ili wafaulu kwani kwa sasa shule za mkoa huo zinafanya vibaya kwenye matokeo ya mtihani.

Rutahinfwa amesema hayo leo wakati anazungumza na walimu wakuu wa shule za msingi, Wakuu wa shule za sekondari, maofisa elimu na viongozi wa ngazi mbalimbali wa sekta ya elimu mkoa wa Dar es Salaam na hasa wa Manispaa ya Ilala jijini.

"Mwalimu mkuu wa shule ya msingi na mkuu wa shule sekondari ndiko mamkalaka ya nidhamu yanakoanzia kwa maana kwenye ngazi za shule,hivyo nitoe mwito walimu wakuu na wakuu wa shule chukueni hatua kwa walimu wanapokosea.

"Mwalimu hata akiwa mke wa kiongozi achukuliwe hatua pale anapokiuka nidhamu,anapokuwa kwenye majukumu yake ni mwalimu na akirudi nyumbani ndio atabaki kuwa mke wa kiongozi.

"Hivyo hakuna sababu ya kuogopa kuchukua haua kwasababu mwalimu aliyekosea ni mke wa mkubwa.Tufuate sheria na kanuni za utumishi wa umma na zile za Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania.Anayekosea aanywe, apewe karipio na akiendelea achukuliwe hatua zaidi,"amesema  Rutahinfwa .

APIGA STOP KUWAPIGA WANAFUNZI
Wakati huo huo umuhimu wa walimu kutomdhuru mwanafunzi kimwili na mwalimu kutembea na kiboko maeneo ya shule hairuhusiwi na kufafanua zipo sheria na kanuni inayosimamia uchapwaji viboko.

"Viboko ambavyo mwanafunzi anatakiwa kuchapwa ni vinne na viandikwe, hakuna  sababu ya kumchapa mwanafunzi na kama kuna ulazima basi anayetakiwa kumchapa mwanafunzi basi awe mwalimu mkuu.Badala ya kuchapa tumieni mbinu mbadala ambayo itafanya mwanafunzi ajutie kosa alilofanya na si kumpiga viboko,"amesema  Rutahinfwa .

ACHENI KUWAANDIKIA NOTISI WANAFUNZI
Pia amewashauri walimu  kuacha tabia ya kujikita kuwaandikia notisi wanafunzi na badala yake kujenga utaratibu wa kuwa na mbinu mbadala ya kufundisha wanafunzi kwa kuwajengea uwezo wa kufikiria na kujenga hoja badala ya kukariri kwa kutumia notisi.

Ametoa mifano mbalimbali katika kuwajengea hoja walimu kubadilika katika ufundishaji na kufafanua yeye akiwa mwalimu wa Shule ya Azania wanafunzi walikuwa wanafaulu na shule kusifika lakini siku hizi shule hiyo haifanyi vizuri katika ufaulu.

"Shule za msingi walimu wanafundisha na ndio maana walimu wanafaulu mtihani wa darasa.Kwa shule z sekondari za mkoa wa Dar es Salaam nahisi kuna tatizo, walimu huenda baadhi yenu hamfundishi na matokeo yake wanafunzi wanafeli.Niwaombe walimu fundisheni wanafunzi wafaulu.Jukumu namba moja la mwalimu ni kufundisha ,hivyo fundisheni,"amesema  Rutahinfwa .

AELEZA MAJUKUMU YA TUME
Winfrida amesema Tume ya Watumishi wa Walimu Tanzania ipo kwa mujibu washeria na ilianza rasmi mwaka 2016 na kufafanua tume hiyo ndicho chombo mamlaka ya nidhamu ya walimu wa shule za msingi na sekondari.

"Asilimia 60 ya watumishi wa umma ni walimu, hivyo walimu ni jeshi kubwa na Serikali kwa kuliona hilo iliamua kuanzisha Tume ya Utumishi ya Walimu kwa ajili ya kusimamia mambo ya walimu na hasa nidhamu.Hivyo masuala yote yanayohusu nidhamu yaafanywa na tume hii,"amesema 

Hivyo amesema hata uamuzi ambao utatolewa na tume hiyo unapaswa kuheshimiwa na anashangaa kuona kamati ya nidhamu ya shule inaamua jambo halafu anatoa diwani au ubunge au mwanasiasa yoyote mwingine anapinga.Hii si sawa lazima tume iheshimiwe.

"Tunafahamu Mkurugenzi ndio ayemuajiri mwalimu na ndio anayelipa mshahara na marupurupu mengine lakini inapofika suala ka nidhamu mkurugenz hana nafasi bali ni Tume ya Utumishi wa Walimu,"amesema. 

Baadhi ya walimu walimi wakuu wa shule za msingi,wakuu wa shule za sekondari,waratibu wa elimu na maofisa elimu mkoa wa Dar es Salaam wakiwa wamesimama kumkaribisha Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania Winfrida Rutahinfwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad