HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 30 April 2018

WAZIRI WA MADINI AAGIZA RIPOTI YA TEITI IPELEKWE KWA CAG KWA AJILI YA UCHUNGUZI

*Ni baada ya kubainika kwa tofauti ya zaidi ya Shilingi bilioni 30 ambayo ni pungufu ya fedha ambayo Serikali imekiri kupokea.

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WAZIRI wa Madini Angella Kairuki amezindua rasmi Ripoti ya Nane ya Taasisi ya Uhamasishaji uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini mafuta na gesi asilia nchini Tanzania(TEITI) kwa mwaka 2015/2016 ambayo inazungumzia ulinganishi wa mapato  ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia huku akitoa maagizo  kwa taasisi hiyo kuhakikisha ripoti hiyo inapelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) baada ya kubainika kuna tofauti ya  zaidi ya Shilingi bilioni 30.
Amefafanua Ripoti ya TEITI inaonesha kuwa kuanzia Julai 1 mwaka 2015 hadi Juni mwaka 2016 kunaonesha jumla ya Sh.434,627,874,380 zimepokelewa serikalini kutoka kampuni 55 za madini , mafuta na gesi asilia zilizoshiriki kwenye mchakato huo wa ulinganishi ambapo kampuni hizo zinaonesha zililipa  serikalini Sh 465,164,747,725 na hivyo kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni pungufu Sh 30,536,873,345 chini ya fedha ambazo Serikali inakiri kupokea.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Waziri Kairuki amepongeza kazi nzuri ya TEITI ya kukamilisha ripoti hiyo lakini ni lazima ifahamike imekuaje imejitokeza tofauti hiyo ya fedha na hivyo ametoa maelekezo taarifa hiyo ipelekwe kwa CAG kwa ajili ya uchunguzi kama kifungu 18(1) cha sheria ya TEITI ya mwaka 2015 kinavyotoka.
"Tunataka hii ripoti iende kwa CAG ili tujue nini ambacho kimetokea na ni vema kazi hiyo ikafanyika kwa wakati,"amesema Waziri Kairuki.
Pia amesema ripoti hiyo  inaonesha sekta ya madini imechangia kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta na gesi asilia ikionesha kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali kwa mwaka 2015,2016.
Amefafanua kuwa yote ambayo yamependekezwa na kamati ya TEITI yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kuhakikisha yale ambayo yamesemwa yanafanyika kama ambavyo wamependekeza kwa maslahi ya Watanzania wote huku akielezea hatua kadhaa ambazo Serikali inachukua kuhakikisha madini yananufaisha wananchi wote.
Waziri Kairuki ameeleza nchi yetu ilijiunga katika mpango wa kimataifa wa Uwazi katika sekta ya uchimbaji wa rasilimali ambapo lengo lake kuu lilikuwa kuhakikisha mapato yanayopatikana katika sekta hiyo yanajulikana wazi kwa wananchi bila kificho.Hivyo  Serikali na kampuni za madini yanawajibika kutoa taarifa zake kwa umma ili ufahamu kilichopatikana na hatimaye wataweza kuhoji ni kwa namna gani wanafanufaika na rasilimali hizo.

"Hivyo Serikali na kampuni ya madini yanajukumu la kutoa taarifa zao kuhusu kilichopatikana katika uchimbaji wa madini, mafuta na gesi katika kipindi husika .Nichukue fursa hii kuipongeza TEITI kwa kazi nzuri ambayo wameifanya tangu mwaka 2001 walipoandaa taarifa ya kwanza  hadi leo hii tumefikia kuzindua taarifa ya nane.Kwa hakika  wamekuwa wakifanya kazi nzuri.Rai yangu kwa wadau wote tuisome taarifa hii kwani itatupa  picha halisi  ya kinachoendelea katika sekta ya madini.

"Sote tunafahamu umuhimu wa sekta ya madini nchini na Serikali ya Awamu ya tano  chini ya  Rais Dk.John Magufuli  ina dhamira ya dhati kuona sekta ya madini inawanufaisha Watanzania wote kwa kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki .Hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria ya madini na kanuni zake na hatua nyingine ambayo endelevu ni kufanya tathimini ya jinsi gani nchi yetu inapata mapato yake kutokana na sekta ya madini kutokana na hatua zilizochukuliwa,"amesema.
Ameongeza jukumu hilo linafanywa na taasisi mbalimbali za Serikali lakini TEITI nayo inatekeleza jukumu hilo kwa uwazi na taarifa zake zinazotolewa kwa wananchi na wadau mbalimbali katika Serikali ,sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali na kufafanua ripoti ya leo ambayo ameizindua imezingumzia mambo mengi ya msingi na lazima yafanyiwe kazi ikiwemo ya kujua kuhusu utofauti wa fedha ambayo imebainika kwenye ripoti ya TEITI.
Waziri Kairuki  ametumia fursa hiyo kuzihakikishia kampuni zote kwamba Serikali inathamini mchango wao katika sekta ya madini nchini  na kuyaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa sheria na kanuni mpya za madini.Hivyo wamekaribisha kampuni nyingine za madini ya ndani na nje ya nchi yaje kuwekeza nchini katika sekta ya madini."Tangu tupitishe sheria mpya ya madini na kanuni zake  zimejitokeza na kuonesha nia ya kuwekeza sekta ya madini nchini.

Amesema hiyo inathibitisha uwazi katika sekta ya madini ni jambo la msingi na lenye manufaa kwa Serikali na kampuni kuhakikisha kila upande unanuifaka na kuomba kampuni kujitokeza kuomba kuwekeza , kutokana kuteuliwa kwa Tume ya Madini na kwamba mchakato wa kushughulikia maombi yao litafanyika mapema iwezekanavyo ili hatua za uwekezaji kuanza.

MALENGO YA TEITI NA UMHIMU WA RIPOTI
Kwa mujibu wa kamati ya TEITI ni kwamba malengo na umuhimu wa ripoti hiyo ni Imeelezwa ni kuboresha Uwazi katika Ukusanyaji na Matumizi  ya  Mapato yanayotokana na Uchimbaji wa Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Kuboresha na kukuza Mchango unaotokana na kodi zinazolipwa  kwa Serikali na makampuni  ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia , Kupunguza Rushwa na matumizi mabaya ya mapato yanayotokana na malipo ya kodi za makampuni ya madini, mafuta na Gesi Asilia  na Kuhamasisha mijadala kwa kutumia takwimu (zilizohakikiwa) zinazotolewa katika Ripoti za TEITI juu ya  mapato na manufaa yanayopatikana kutokana na uchimbaji wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia.

UBORA WA RIPOTI  ZA TEITI
Imeelezwa ni Usimamizi wa Maandalizi ya Ripoti za EITI unafanywa kupitia Kamati ya EITI  inayoundwa na na wajumbe kutoka Makampuni, Asasi za Kiraia na Taasisi za Serikali, Takwimu za kodi na Mapato zinakusanywa kutoka katika Hesabu zilizokaguliwa na wakaguzi wa Nje wa makampuni; na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Taasisi za Serikali, Takwimu uhakikiwa na ulinganishaji hufanywa kati ya takwimu za malipo ya kodi na maduhuli yaliyopokelewa ,Taasisi husika na tofauti huchunguzwa na taarifa ya uchunguzi huwekwa wazi kwa wananchi, hii ni pamoja na hatua zilizochukuliwa endapo CAG atabaini vitendo vya Upotevu au udhaifu katika ukusanyaji wa mapato na Kamati ya EITI hutakiwa kuchukuwa hatua kuondoa kasoro zilizobainishwa katika Ripoti  na kuonyesha matokeo juu ya uboreshaji wa uwazi na uwajibikaji  katika ulipaji na ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Rasilimali hizo.
UWAZI KATIKA UVUNAJI WA RASILIMALI
Imefafanuliwa kuwa unazingatiwa katika maeneo yafuatayo ambayo ni ulipaji wa Kodi, Mrahaba na Ada, Ukusanyaji wa Mapato na  Mgawanyo na matumizi ya mapato.Kuhusu  uchambuzi wa takwimu za kodina mrahaba ripoti imefafanua kampun 1287 yalijishughulisha katika uchimbaji na utafutaji wa Madini,Mafuta, na Gesi asilia 2015/16 na mapato ya Sh 547, 171, 999,937.05 kutoka makampuni hayo (1287) yalikusanywa na Serikali. Wakati kampuni 55 yalichangia asilimia  95.05  ya makusanyo na kampuni 1232 yalichangia asilimia 4.95  ya makusanyo.

Imeelezwa Uhakiki wa Malipo ya kampuni 55 na Mapato yaliyopokelewa na Taasisi za Serikali ni kwamba kampuni  55 yalionyesha yamelipa Sh.465,164,747,725, Serikali imekiri kupokea Sh    434,627,874,380 na kati hizo tofauti  Sh.30,536,873,345 ambayo ni sawa na asilimia  7  ya Mapato yote kutoka Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inaelezwa tofauti za malipo na mapato zinaweza kuwa zimechangiwa  na TRA  imekusanya chini kwa kiasi  cha Sh  25,562,261,234.41 ikilinganishwa na malipo ya kampuni, Wizara ya Madini imekiri kupokea zaidi ya kiasi kilicholipwa na Makampuni kwa Sh  4,717,501,333. 54. Hiyo  imetokana na baadhi ya kampuni zilizolipa zimeshindwa kuripoti au zimefunga ofisi zao hapa nchini, TPDC imekusanya chini ya kiasi kilichoripotiwa na Makampuni kwa Sh. 2,749,470,555.00

Pia Msajili wa Hazina hakuripoti gawio la Serikali, wakati STAMICO wameripoti kulipa gawio Hazina la Sh. 1,396,229689.00, Halmashauri (Local Governments)  zimekiri kupokea Ushuru wa Huduma (Service levy)  kwa kiasi cha Sh. 1,250,571,117.13 wakati makampuni yameonyesha kulipa shilingi 7,364,633,037.64. Hiyo inaleta  tofauti ya Sh. 6,114,061,920.51

Kuhusu mambo makuu katika Ripoti Ya TEITI Ya Mwaka 2015/2016 inaonesha Mapato yaliyokusanywa kutoka makampuni ya Madini, Mafuta na gesi Asilia ni Sh.bilioni  547 bilioni, kiasi hicho ni 0.74% ya Mapato yote ya kodi  kwa Serikali (Sh.trilioni  74.073), Thamani ya Mauzo ya Madini Nje ya Nchi ni TzS 3.582 trilioni, Mapato yanayotokana na kodi pekee ni madogo, Jitihada za kufungamanisha shughuli za makampuni ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia  na Sekta nyingine hazina budi kuendelezwa.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya nane ya TEITI  ya ulinganishi wa Mapato ya Serikali na Malipo ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 leo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi wa Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini Mafuta na Gesi Asilia nchini Tanzania(TEITI), Augustina Rutahiwa akizungumzia mchakato ulivyofanyika ili kupata ripoti iliyonzuri wakati wa uzinduzi wa ripoti ya nane ya TEITI  ya ulinganishi wa Mapato ya Serikali na Malipoya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akizungumzia serikali ivyojipanga kulinda madini ya hapa nchini kuwanufaisha hasa wazawa wakati wa mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya nane ya TEITI uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Msimamizi wa kujitegemea, Symphorian Malingumu akiwasilisha ripoti ya nane ya TEITI  ya ulinganishi wa Mapato ya Serikali na Malipo ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 leo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ripoti ya nane ya TEITI  ya ulinganishi wa Mapato ya Serikali na Malipo ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 leo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila pamoja na baadhi ya wajumbe kutoka Makampuni, Asasi za Kiraia na Taasisi za Serikali wakiwa wameshika ripoti ya nane ya TEITI  ya ulinganishi wa Mapato ya Serikali na Malipo ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16  mara baada ya kuzinduliwa leo.
 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila wakiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe kutoka Makampuni, Asasi za Kiraia na Taasisi za Serikali walioshiriki katika mchakato wa ripoti  ya nane ya TEITI  ya ulinganishi wa Mapato ya Serikali na Malipoya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 leo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad