HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 6, 2018

Serikali kuwashughulikia wanaovamia vyanzo vya maji

Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi
Serikali mkoani Shinyanga imesema itawashughulikia wanaovamia kufanya shughuli za kilimo na kunywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji na kusababisha ongezeko la uharibifu wa mazingira.
Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Zainab Telack amesema hayo leo katika kijiji cha Songwa wilayani Kishapu wakati wa siku ya pili ya maadhimisho ya upandaji miti kitaifa yanayoendelea.
Alionya kuwa shughuli hizo zinahatarisha uhai wa vyanzo hivyo vya maji pamoja na uhai wa binadamu kutokana na matumizi ya madawa yanayotumika katika kilimo hicho.
“Kishapu mna mabwawa matatu lakini kwa bahati mbaya wachimbaji almasi na wanaolima kando kando mmeyaharibu ninyi wenyewe kwa hiyo niwaombe kwa sababu tumetambua kuchimba kwenye mabwawa ni makosa na kulima ni makosa pia ni marufuku kufanya shughuli hizo,” alisisitiza.
“Mnapofanya kilimo cha nyanya au mahindi mnatumia madawa yenye sumu na kuyachafua maji kwa hiyo hayafai kutumika kwani siku hamna maji mnayatumia wakati huo mmeweka sumu, mnaogesha watoto wanapata madhara, acheni kulima kando ya mabwawa haya,” aliongeza.
Aidha, Mhe. Telack alisisitiza umuhimu wa kupanda miti kando ya vyanzo vya maji hasa mabwawa na kuwa ndiyo chanzo cha maji kwani husaidia yasikauke hivyo huwezesha mvua kunyesha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe Nyabaganga Taraba alisema hapo nyuma wananchi hawakuwa na mwamko katika shughuli za uhifadhi mazingira hivyo kuchangia kuwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Taraba alisema kuwa baada ya kupanda miti katika maeneo yanayozunguka bwawa hilo hatua hiyo imeweza kusaidia kurudi upya kwake na hivyo wananchi kuendelea kupata faida.
Alisisitiza kuwa suala la upandaji miti pamoja na utunzaji misitu ni la wananchi wote na ndio maana viongozi wote wanashiriki katika zoezi na kuahidi viongozi watandelea kuwa bega kwa bega kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,  Zainab Telack akizungumza na wananchi wa Songwa mara baada ya kuongoza zoezi la kupanda miti kandokando mwa bwawa la Mhumbu ikiwa ni mojawapo ya maadhimisho ya Upandaji miti kitaifa wilayani Kishapu. 
 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza wananchi wa Songwa mara baada ya zoezi la kupanda miti kandokando mwa bwawa la Mhumbu ikiwa ni mojawapo ya maadhimisho hayo.
Watumishi kutoka Hamashauri ya Wilaya ya Kishapu wakImwagilia miche ya miti iliyopandwa wakati wakiendelea na zoezi la upandaji miti kando mwa bwawa la Mhumbu kijiji cha Songwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad