HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 16 April 2018

MAZINGIRA YA UWEKEZAJI SEKTA YA FEDHA VIJIJINI KUBORESHWA

Na: WFM
Serikali imeahidi kuboresha miundombinu na fursa nyingi za kiuchumi katika maeneo ya vijijini ili kuweka mazingira bora na salama yatakayovutia wawekezaji katika sekta mbalimbali hususani Sekta ya Fedha.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kalenga (CCM) Mhe. Godfrey Mgimwa aliyetaka kujua tamko la Serikali juu ya idadi kubwa ya benki za biashara kufunguliwa kwenye miji mikubwa.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa miji mikubwa inakidhi vigezo muhimu vya uwekezaji kwa Sekta ya Fedha kama vile uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi, miundombinu ya kisasa na usalama ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.

Alisema kuwa kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi nchini unaotekelezwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, shughuli nyingi za kiuchumi hususani benki zinaendeshwa na Sekta Binafsi .

“Kwakuwa Sekta Binafsi lengo lake ni kufanya biashara na kupata faida, uwanzishaji wa huduma za kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia fursa za kiuchumi zilizopo katika eneo husika, uwepo wa miundombinu wezeshi na usalama”, alisema Dkt. Kijaji.

Alifafanua kuwa Serikali inachokifanya ni kuweka mazingira bora yatakayowavutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza maeneo ya vijijini kwa kuwa lengo ni kufikisha huduma za kifedha kwa watanzania wote.

Katika swali la nyongeza la Mbunge huyo, alitaka kujua mbinu mbadala ya Serikali kuhakikisha inapeleka huduma za benki vijijini, kwa kuwa mpaka sasa Serikali bado haijaunda Sera ya kuhakikisha huduma hizo zinawafikia walengwa hasa wa vijijini.

Dkt. Kijaji alieleza kuwa mpango mbadala wa kuhakikisha huduma za kibenki zinafika vijijini upo na Serikali inausimamia vizuri, na kuongeza kuwa mpango huo umeiwezesha Tanzania kuongoza katika huduma za fedha jumuishi barani Afrika.

Aidha Dkt. Kijaji alifafanua kuwa uwepo wa mawakala wa benki, kutolewa kwa huduma za kibenki kupitia Kampuni za simu ni ishara tosha kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad