HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 6, 2018

MAHAKAMA YAUTAKA UPELELEZI KESI VIGOGO WA SIX TELECOMS

Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa  mashtaka ifikapo Aprili 20 mwaka huu upeleke taarifa nzuri ya upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wanne wa Kampuni ya Six Telecoms Limited akiwemo Mhadhiri na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ringo Willy Tenga.

Akizungumza leo mahakamani hapo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema wanahitaji kesi hiyo isichukue mwaka mzima ikiwa haijatolewa maamuzi, ifike mahali ijulikane washtakiwa kama wanafungwa wafungwe kama wana achiwa waachiwe.

Simba amesema hayo kutokana na taarifa kutoka kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi Mutalemwa 
Kishenyi kuwa upelelezi bado haujakamilika na jalada lipo kwa  DPP Kwa ajili ya mapitio.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi Alex Mshumbusi aliiomba Mahakama kuamuru upande wa mashtaka tarehe ijayo walete taarifa ya upelelezi umefikia wapi.

Hakimu Simba amesema hizo sababu za upande wa mashtaka zitafikia mahali zitaisha na kuamuru wapelekwe taarifa nzuri ya upelelezi tarehe ijayo ili kesi hiyo isifike mwaka haijatolewa uamuzi.

Washtakiwa hao wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhandisi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya  Six telecoms, Hafidhi  Shamte maarufu Rashidi  Shamte, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Mayunga Noni, Mwanasheria na Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Odeny Chacha na Kampuni ya Six Telecoms Limited. 

Katika kesi hiyo washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya utakatishaji wa fedha ambapo  wanadaiwa   kuwa kati ya Januari 1 mwaka  2014 na Januari 14 mwaka 2016 Dar es Salaam, walitoza maalipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango  cha dola 0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Januari Mosi mwaka 2014 na Januari 14 mwaka 2016 kwa udanganyifu na kwania ya kuepuka maalipo, walishindwa kulipa kiasi cha dola 3,282,741.12 kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama maalipo ya mapato.

Katika shtaka la tatu, inadaiwa kuwa washtakiwa hao katika kipindi hicho cha  kati ya Januari Mosi 2014 na Januari 14 mwaka 2016 walishindwa kulipa ada za udhibiti za dola 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shtaka la nne la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni,Tenga na Chacha wanadaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2014 na Januari 14 mwaka 2016 walijipatia, walitumia ama walisimamia dola 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana Mashtaka yaliyotangulia.

Katika shtaka la tano la utakatishaji fedha, inadaiwa kuwa kampuni ya Six Telecoms Limited kati ya Januari 2014 na Januari 14 mwaka 2016  ilijipatia, ilitumia na kusimamia dola 3,282,741.12 wakati ikijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu yanayotokana Mashtaka yaliyotangulia.

Wakati shtaka la sita, washtakiwa hao  wanadaiwa kuwa waliisababishia mamlaka hiyo ya TCRA hasara ya dola za kimarekani 3,748,751.22, sawa na Sh.bilioni  8 za kitanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad