HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 14, 2018

JESHI LA POLISI LAKAMATA SILAHA,WATUHUMIWA WA UHALIFU 368

Na Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kukamata Silaha mbalimbali na watuhumiwa 368 katika Oparesheni Maalum inayoendelea katika Ukanda wa Kusini unaojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Akizungumza mkoani Mtwara, Mkuu wa Operesheni Maalum za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Liberatus Sabas alisema kati ya watuhumiwa 368, 13 tayari wamefikishwa Mahakamani, 152 wamekabidhiwa Idara ya Uhamiaji kwa hatua zaidi, tisa wapo chini ya Upelelezi na 194 wapo chini ya uangalizi wa Polisi (Police Supervisee).

Sabas amezitaja Silaha zilizokamatwa kuwa ni pamoja na SMG mbili, Pistol tano, Shotgun moja na risasi 145,  Visu 96, Makoti ya Sare za Jeshi la Msumbiji mawili, Raba za Jeshi la Msumbiji jozi mbili pamoja na vifaa vya kutengenezea milipuko. 

“Baadhi ya watuhumiwa ni wale waliokimbia katika Operesheni yetu ya Mkoa wa Kipolisi Rufiji baada ya kuwazidi nguvu na sasa nawaambia tu wajisalimishe kwani hatuna mchezo hata wakimbilie wapi mana tumepata taarifa kuwa wamejificha nchini Msumbiji lakini kule napo wameanzisha operesheni kama hii“. Alisema Sabas.

Aidha Kamanda Sabas amesema Operesheni hiyo  ni endelevu na inashirikisha vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama hivyo ametoa wito kwa raia wema kuendelea kutoa taarifa za siri ili kuendeleza amani na usalama hapa nchini.

Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Polisi la nchini Msumbiji alikutana na IGP Simon Sirro jijini Dar es Salaam kwa lengo kuboresha ushirikiano katika mapambano ya uhalifu unaovuka mipaka ambayo ndio imekuwa changamoto katika nchi mbalimbali.
Mkuu wa Operesheni maalum za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Liberatus Sabas akionyesha baadhi ya Silaha zilizokamatwa katika Operesheni  maalum ya kupambana na uhalifu na wahalifu inayoendelea katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Wengine ni Maofisa mbalimbali waliopo katika Operesheni hiyo. (Picha na Jeshi la Polisi).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad