HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 7 March 2018

TWB yadai mikopo sugu yenye thamani ya Tsh.bilioni 7.9 toka kwa wateja 7,065

Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) katika hatua zake za  kutaka kuimarisha mtaji wake na kufanya kazi zake kwa ufanisi imewataka wateja wake 7,065 wenye mikopo sugu yenye thamani Tsh. bilioni 7.9, kulipa mikopo hiyo ndani ya siku saba vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Bi. Beng’i Issa alisema benki imeanza kuchukua hatua za kuimarisha mtaji wake kwa kuwataka wateja wake wenye madeni sugu kulipa madeni yao ndani ya siku hizo vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa. 

“Moja ya mambo yanayokwamisha  kuimarika kwa mtaji na kupanua huduma za kibenki ni kuwepo kwa mikopo sugu,” sasa tunawataka wateja wetu wenye mikopo sugu kulipa bila shuruti vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa, aliongeza kusema,Bi Issa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha mtaji wa benki unaimrika na itasaidia kutoa huduma za kibenki kwa ufanisi. Wakopaji wengi wamepitiliza siku 90 za urejeshaji madeni ya mikopo yao na hiyo kinyume na utaratibu wa mikataba waliyokubaliana na benki wakati wanakopa.

Pia alisema hatua hiyo ni maagizo ya Benki Kuu (BOT) kama alivyoelekeza Gavana Januari 5, 2018 kuwa benki inahitajika kuongeza mtaji wake kwa kipindi cha miezi sita kinachotarajia  kumalizika Juni 30, 2018.

Akifafanua zaidi alisema agizo hilo linaelekeza benki kukidhi matakwa ya mtaji kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha ya Mwaka 2006.

Bi. Issa alisema tayari kesi nyingine 43 zimefunguliwa mahakamaini kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2017 ambapo benki inadai Tsh. Bilioni 1.870. 

Alisema bodi yake hiyo ina mwaka mmoja na imefanya mambo mengi ya kuiweka menejimenti vizuri, mahesabu na mfumo wa kibenki kufanya kazi vizuri na kwa mara ya kwanza wamepata hati ya ukaguzi safi wa fedha.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Japhet Justine alisema benki yao ipo katika hatua ya kuendelea kupanua huduma zake  hivyo inawataka wenye madeni ya mikopo kulipa madeni yao bila shuruti.

“Tunawataka wateja wetu wenye madeni ya mikopo kufika katika matawi ya benki walipopatia mikopo,” na kwa kufanya hivyo wataiwezesha benki kuendelea na majukumu yake vizuri na kupanua huduma, aliongeza kusema, Bw. Justine.

Alisema benki imeshafanya mabadiliko makubwa katika uongozi kwa upande wa mikopo, hivyo wateja ambao hawatalipa ndani ya siku saba taarifa zao watazipeleka BOT Credit Reference Bureau ambako hawataruhusiwa tena kupata mikopo katika benki nyingine, alisema, Bw. Justine.

Alisema wadaiwa hao wapo katika maeneo ya Dar es Salaam, Songea, Makambako, Mbeya, Iringa, Dodoma na Mwanza, na aliongeza kusema kuwa wadaiwa wakubwa wa mikopo hiyo wapo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi wa Benki ya Wanawake (TWB), Bi. Beng’i Issa akisisitiza jambo wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya benki hiyo ilivyojipanga kuimarisha mtaji wake kwa kuwataka wateja wake wenye madeni sugu kulipa madeni yao ya mikopo, wa pili kulia ni Mjumbe wa Bodi hiyo, Bw. Oswald Mutaitina, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Japhet Justine na wa pili kushoto ni Mjumbe wa Bodi hiyo Bw. Ramadhani Saidi. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad