HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 13 March 2018

TPA yaongeza biashara kati ya Tanzania, Malawi kwa kuongeza meli

Na Mwandishi Wetu
KUANZA safari kwa meli za mizigo za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika nchi ya Malawi kutaongeza wigo wa kibiashara kati ya nchi ya Tanzania na Malawi.

Mbali ya kuongeza zaidi wigo wa biashara kati ya nchi hizo, meli hizo – MV Njombe na MV Ruvuma pia zinatarajiwa kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili za Tanzania na Malawi.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Balozi Benedicto Mashiba wakati akipokea kwa mara ya kwanza ujio wa meli nyingine ya TPA, MV Ruvuma katika bandari ya Monkey Bay nchini Malawi.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Balozi Mashiba amesema kwamba kama bidhaa zitafika Malawi au Tanzania kwa wakati na haraka na kwa unafuu zaidi.  Mheshimiwa Balozi aliendelea kueleza lwamba watumiaji wataongezeka na wakishaongezeka basi hata uzalishaji viwandani pia unaongezeka.

Kwa  upande wa Serikali zote mbili, nazo zitanufaika kwa kutoza kodi ambayo itaongeza mapato ya nchi, pia Balozi Mashimba ameongezea kwamba kwa kuwa viwanda hivi vinatumia malighafi kutoka mashambani, hii ina maana kwamba hata wakulima nao watanufaika.

Kwa Serikali zote mbili za Tanzania na Malawi, hilo ni jambo ambalo linalitajika kabisa, ili uchumi uendelee kukua na hatimaye wananchi wote waweze kunufaika na Serikali kwa maana ya kupata ushuru na tozo mbalimbali.

Naye Kaimu Naibu Mkuu Mkurugenzi upande wa Huduma wa TPA, Bibi Francisca Muindi amesema kwamba wao kama TPA wanawakaribisha sana wafanyabiashara wa nchini Malawi na Tanzania kutumia meli zote mbili za MV Ruvuma na Mv Njombe kwani ni nafuu na za uhakika zaidi kusafirisha bidhaa.

Amesema kwamba meli hizi mbili zitakuwa zikitumika kubeba mizigo si tu ya Tanzania na mikoa inayozuunguka ziwa hilo bali pia kupeleka mzigo Malawi na Msumbiji kwa bei nafuu zaidi, ikilinganishwa na usafiri wa aina nyingine, kama vlle barabara.

Hivyo, Bibi Muindi ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nchi zote mbili kwamba badala ya kutumia barabara kupeleka mizigo yao nchini Malawi, watumie njia ya maji kwani ni ya uhakika, nafuu na haraka zaidi.

Ama kwa hakika, TPA ilieleza kwamba kwa kutumia meli hizo itawasaidia wafanyabiashara kunufaika kutokana na unafuu na usalama wa kusafirisha mizigo na hatimaye kuongeza faida kwenye biashara zao.  Jumuia za wafanyabiashara wa Tanzania na Malawi zimehamsishwa kutumia meli hizo kwa faida ya Serikali za nchi zote na vile vile kwa faida ya wafanyabiashara ili kupunguza gharama za usafirishaji; na hatimaye walaji wa mwisho kuweza kupata mahitaji yao kwa bei nafuu.

Meneja Utekelezaji wa Kampuni ya Meli ya Malawi, Capt. Francis Chilalika, kwa upande wake amesema kwamba bidhaa ambazo huwa wanasafirisha mara kwa mara kutoka Tanzania kuja nchini Malawi ni ‘Clinker’.

‘Clinker’ ndiyo bidhaa iliyoletwa na meli ya MV Ruvuma nchini Malawi pamoja na shehena ya saruji kutoka kiwanda cha Saruji cha Mbeya kuja kiwanda cha Saruji cha Larfage nchini Malawi.

Nahodha huyo wa Kampuni ya Meli ya Malawi alisema, pamoja na ‘Clinker’, bidhaa nyingine ambazo zimekuwa zikisafirishwa sana kutoka nchini Tanzania kuja Malawi ni pamoja na saruji.  

“Tumekuwa tukihudumia shehena za namna tangu mwishoni mwa mwaka 2016 hadi sasa, kama ujuavyo Malawi tuna mahitaji makubwa sana ya saruji, hivyo hii kwetu tunaiona ni kama biashara endelevu,” amesema.

Akizungumzia bandari ya Chipoka ambayo imejaa mchanga kutokana na kina cha maji kupungua, Nahodha huyo amesema kwamba wapo katika mchakato wa kuichimba bandari hiyo.

Amesema kwamba kwa sasa wanafanya utafiti kujua ukubwa wa tatizo ili kujua makadirio ya gharama za  hatimaye kuandaa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa uchimbaji huo.

Bandari ya Chipoka ndiyo iliyo katika nafasi nzuri kwa upande wa usafirisha mizigo nchini Malawi haswa kwa mizigo inayokwenda mji wa Lilongwe.

Meli ya mizigo ya MV Ruvuma ambayo imebeba zaidi ya tani 900 za shehena ya saruji na ‘clinker’ kutoka bandari ya Kiwira, mjini Mbeya, imewasili salama na mapema katika bandari ya Monkey Bay nchini Malawi. 

Hii ni mara ya kwanza kwa meli ya MV Ruvuma kuleta mzigo nchini Malawi na ni mara ya pili kwa meli za TPA kuleta shehena ya mizigo nchini humo. 

Awali meli nyingine ya mizigo ya TPA yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 pia iitwayo MV Njombe nayo ilileta shehena ya zaidi ya tani 800 za saruji katika bandari ya Nkhata Bay nchini Malawi kwa mafanikio makubwa hali iliyowavutia wafanyabiashara wengine kutumia meli ya MV Ruvuma kuleta mzigo nchini Malawi kupitia bandari ya Monkey Bay.  

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad