HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 8 March 2018

Mbunge Chatanda amuomba Mkurugenzi Mji Korogwe kuwaokoa wanafunzi.

Na Yusuph Mussa, Korogwe
MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri,  kutafuta fedha haraka ili kukamilisha ujenzi wa madarasa matatu na ofisi mbili za walimu Shule ya Msingi Msambiazi.

Amesema hayo baada ya kufanya  ziara kwenye shule hiyo leo Machi 8, 2018 na kukuta baadhi ya madarasa ya shule hiyo ni tishio kwa usalama wa wanafunzi, kwani kuta na madirisha vinataka kuanguka, hivyo kufungwa kamba ili kuzuia mabati yasiezuliwe na upepo, huku  mabati hayo yakiwa yametoboka.

Chatanda alisema wasisubiri watoto hao kupata madhara, bali wachukue hatua kwa kumaliza ujenzi wa maboma hayo ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi, Serikali na wahisani.

"Ofisa Ellimu Msingi (Elias Mavoa) naomba umfikishie salamu Mkurugenzi wa Halmashauri (Shauri). Atafute fedha za haraka tumalize madarasa haya, kwani madarasa haya ya sasa ni machakavu na mimi mwenyewe nimeyaona... haiwezekani dirisha na mbao za bati ziwe zimeshikiliwa na kamba.

"Lakini kama alivyosema Mwalimu Mkuu (Zena Machite) wakati anatoa taarifa yake, ndani ya madarasa hayo mvua ikinyesha kunavuja na inabidi kuhamisha wanafunzi kwenye madarasa hayo wakati wa mvua" alisema Chatanda.

Mkuu wa Shule Machite, alisema moja ya changamoto kwenye shule hiyo ni uchakavu wa madarasa matatu na ofisi mbili, ile ya Mwalimu Mkuu na Ofisi ya Walimu.

Machite alisema mpaka sasa ujenzi wa madarasa hayo matatu na ofisi mbili za walimu umegharimu sh 12,898,000 na hadi kukamilika utagharimu sh. milioni 44.1. Na baadhi ya wadau waliochangia ni jamii sh. milioni 1.9, Mfuko wa Jimbo sh. 575,000, harambee ya wadau wengine sh. 423,000 na fedha kutoka halmashauri sh. milioni 10.

Machite alisema wanajenga choo kipya chenye matundu 10 kutokana na choo kilichopo kuwa chakavu na kuhatarisha afya na usalama wa wanafunzi, kwani wakati wowote kinaweza kuanguka.

Alisema hadi sasa ujenzi umebakia umaliziaji ambapo ni milango na madirisha ya vyoo na rangi kwenye baadhi ya maeneo, ambapo hadi sasa ujenzi wa choo hicho umetumia sh. milioni 9.8, na ili kukamilisha kunahitajika sh. milioni 1.5.

Hata hivyo Chatanda ameahidi kumalizia ujenzi wa choo hicho kwa kutoa sh. milioni 1.5 kupitia Mfuko wa Jimbo,  huku Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Mavoa akimshukuru Chatanda kwa kutoa sh. milioni 1.5 kumalizia ujenzi wa choo.
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda (kulia) akikagua majengo ya madarasa mapya matatu na ofisi mbili za walimu Shule ya Msingi Msambiazi, Kata ya Mtonga katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Kushoto ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Zena Machita. (Picha na Yusuph Mussa).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad