HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 7, 2018

KAMPUNI YAMPA BAISKELI MWANAFUNZI WA DARASA LA SABA ILI ATIMIZE NDOTO YAKE

Na Mwandishi wetu
KAMPUNI ya D&G Export Company Ltd inayojishughulisha na ununuzi wa mazao na utunzaji wa korosho wilayani Tunduru na Liwale imeamua kumsaidia baiskeli ya magurudumu matatu mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Kichangani Shaibu Mpoto.

Mwanafunzi huyo alishindwa kuendelea na masomo yake baada ya kupata ugonjwa  wa kupooza miguu, miaka minne iliyopita jambo ambalo lilimfanya kuwa na wakati mgumu kuendelea na masomo lakini  kupatikana kwa baiskeli hiyo kutarudisha ndoto zake kielimu.

Shaibu alipatwa na tatizo la kupooza mwaka 2014 akiwa darasa la tatu na alilazimika kukaa nyumbani bila kujua hatma yake.Hivyo Kampuni hiyo kupitia Mkurugenzi wake Geofrey Kalamba imeamua kutoa msaada wa baiskeli hiyo yenye thamani ya Sh.320,000.

Akizungumzia zaidi leo kuhusu msaada huo, Kalamba amesema ametoa baiskeli hiyo ili kumsaidia Shaibu kuhudhuria masomo na hatimaye aweze kutimiza ndoto zake.

"Niliguswa sana baada ya kuona amebebwa mgongoni na bibi yake akipelekwa shuleni licha ya umri wa Shaibu kuwa mkubwa.Hivyo nilisema lazima nimsaidie baiskeli ili kumrahisisha anapotaka kwenda shuleni na maeneo mengine,"amesema.

Kwa upande wake Shaibu amesema ameshukuru kwa kupata msaada huo na kueleza ndoto za kupata elimu zitatimia kwani alishakata tamaa lakini sasa anauhakika atatimiza alichokusudia kwenye elimu.

"Nashukuru sana kwa msaada huu wa baiskeli, itanisaidia kwenda na kurudi shuleni na kwenda katika maeneo mengine bila kuhitaji kubebwa na mtu.Kila siku nilikuwa na mhurumia bibi yangu ambaye alilazimika kunibeba  kunipeleka shule na kunirudisha nyumbani,namuomba Mungu ampe maisha marefu bibi yangu na  aliyenipa baiskeli,"amesema Shaibu.

Kwa upande wake mlezi wa Shaibu ambaye ni bibi yake Fatma Kaluma amesema kwa sasa atapumzika kumbeba Shaibu kila siku asubuhi na jioni na atapata muda wa kufanya kazi za kujiongezea kipato kwa kuwa awali alishindwa kupata nafasi hiyo kutokana na tatizo la mjukuu 
wake.

Amewaomba wasamaria wema kuendelea kumsaidia mjukuu wake, kwani bado anahitaji vifaa vya shule ikiwemo daftari,vitabu na hata sare za shule ili mjukuu wake aweze kutimiza ndoto za kupata elimu.
 Mkurugenzi wa kampuni ya D&G Export Company Ltd, Geofrey Kalamba (kushoto) akimkabidhi baiskeli ya magurudumu matatu kwa mlezi wa mwanafunzi, Shaibu Mpoto anayesoma darasa la 7 shule ya msingi Kichangani Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ili iweze kumsaidia kwenda shuleni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad