HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 8, 2018

Tambwe Hizza wa Chadema Afariki Dunia

Mwanasiasa mkongwe na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tambwe Hizza amefariki dunia asubuhi ya kuamkia leo (Alhamis ) akiwa nyumbani kwake kwa ugonjwa wa pumu.


Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene amethibitisha kifo hicho akisema Hiza amefariki leo asubuhi nyumbani kwake Mbagala akiwa amelala.


Hiza amefariki kipindi ambacho alikuwa katika timu ya kampeni za kumnadi mgombea wa ubunge wa Chama hicho katika Jimbo la Kinondoni, Salumu Mwalimu na jana jioni alipanda jukwaani kumnadi.

Mwalimu akizungumzia kifo hicho amesema “sina maneno yanayoweza kumwelezea Tambwe, Tambwe alikuwa mtu muhimu sana katika timu yangu ya kampeni, kaniacha kipindi muhimu sana.”

“Alikuwa nguzo yangu, katika muda aliokuwa nasi ndani ya chama Tambwe alikuwa na ushawishi mkubwa sana, hadi jana saa 4 usiku tulikuwa sote, Tambwe kaniacha kipindi muhimu kweli kweli sijui hata niseme nini,” ameongeza Mwalimu

Kuhusu kuendelea na kampeni, Mwalimu amesema “mimi binafsi sidhani kama nitaweza, lakini ngoja nisubiri chama, kwa sasa nakwenda msibani ila baadae tutajua.”

Mwaka 2015, Hiza alitangaza kujiunga na Chadema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu akitokea CCM ambako aliwahi kuhudumu kama mkuu wa kitengo cha propaganda wa chama hicho tawala.

Kabla ya kujiunga na CCM alihama kutoka katika Chama cha Wananchi (CUF) ambako pia alihamia kutoka NCCR-Mageuzi.

Katika kampeni za urais 2015, Hiza alikuwa katika jopo la kumnadi mgombea wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa na mara zote alikuwa anapanda jukwaani mwanzoni kama alivyokuwa akifanya kwenye kampeni za  Mwalimu zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad