HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 28 February 2018

FARM AFRICA YAHAMASISHA WAKULIMA WADOGO WA NAFAKA KUTUMIA MITANDAO KUPATA MASOKO YA MAZAO

Na Mwandishi Wetu, Arusha
Shirika la Kimataifa la Farm Africa limewataka wakulima wadogo wa mazao ya nafaka hapa nchini kutumia mifumo ya mitandao kupitia simu za mkononi kutangaza bei ya mazao ya nafaka na kupata taarifa za kilimo bora ili kuwasaidia kupata kipato chenye tija na kuondokana na hali duni katika familia zao.

Meneja Program ya FoodTrade wa Shirika hilo la Kimataifa la Farm Africa,Bi. Beatrice Muliahela alisema hayo jijini Arusha katika warsha ya siku moja kuwa wakulima wadogo wanahitajika kutumia mifumo ya mitandao kupitia simu katika kutangaza bei ya mazao yao na kupata taarifa za kilimo bora ili kuwasaidia kupata kipato chenye tija na kuondokana na hali duni katika familia zao.

Mradi huu ni wa miaka miwili na unafadhiliwa na Department for International Development (DFID) kupitia DAI kwa kuhusisha wadau wengine kama Taasisi ya Maendeleo Vijijini na Mijini (RUDI) na VECO kwa sasa Rikolto ambao umesaidia wakulima wadogo 70,000 nchini Tanzania na Uganda.

“Farm Africa inahitaji kuona wakulima wadogo nchini Tanzania wanatumia mifumo ya mitandao kupitia simu katika kutangaza bei ya mazao yao na kuuza kwa bei nzuri zaidi,” na hii tunahamasisha katika nchi zote kumi za Afrika Mashariki kutumia mifumo hii, aliongeza kusema,Bi. Muliahela.

Alisema Farm Africa inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau wake ambao wamejikita katika kusaidia wakulima wadogo wa kilimo cha mazao ya nafaka kupata soko nzuri na pia kupata taarifa za masoko na elimu ya namna ya kuzalisha mazao.

Aliitaja mifumo hiyo ni G- Soko, E-Soko na Ninayo ambayo imeleta huduma za taarifa za masoko kwa wakulima kwa kutumia mitandao kupitia simu za mkononi.

Pia alisema mifumo hiyo inaenda sambamba na mifumo ya kuweka mazao yao katika maghala ambapo kwa umoja huo, uongozi wa ghala unaweza kutangaza tani za mazao iliyopo, ubora wa mazao na bei kwa ajili ya kupata soko la uhakika.

Bi. Muliahela alifafanua kwamba mifumo hiyo ya kisasa inasaidia wakulima kuondokana na mifumo ya awali ambayo wanunuzi walikuwa wanaenda moja kwa moja shambani na kununua mazao kwa bei wanazo taka wao na wakulima kukosa faida halisi ya mazao yao.

Wadau wengine ambao shirika hilo linafanya nao kazi katika kuinua kilimo cha nafaka na bei zake ni pamoja na RUDI, VECO Rikolto, DAI, Baraza la Nafaka Afrika Mashariki (EAGC) ambapo ambapo mazao ya nafaka ni pamoja na mahindi, mpunga na maharage.

Awali Mkurugenzi wa Msaidizi Kitengo cha Kuzuia Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno Wizara ya Kilimo, Bi. Josephine Omolo  akifungua warsha hiyo alisema serikali itaendelea kushirikiana na Farm Africa pamoja na wadau wake kuhakikisha mifumo hiyo inasaidia wakulima kupata masoko ya uhakika na ya bei nzuri.

“Serikali imekuwa ikiweka mifumo bora ya kuimarisha kilimo na masoko ya mazao na hii imesaidia kupata mazao ya chakula ya kutosha na kwa ajili ya biashara,” na hii mifumo imekuja kuongeza nguvu katika kuyafikia masoko ya nje, aliongeza kusema,Bi. Omolo.

Pia alitolea ufafanuzi kwamba serikali haijaweka zuio la kuuza mazao ya chakula nje ya nchi bali inapojiridhisha nchi inachakula cha kutosha na kinachobaki kinaruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.

Naye Afisa Program Kitengo cha Masoko Rasmi wa Baraza la Nafaka Africa Mashariki (EAGC), Bw. Prudence Mushi alisema G-Soko ni mfumo wa kieletroniki kupitia mtandao wa simu ambao wakulima wanaweza kuutumia kutangaza bei ya mazao yao, kuwasiliana na mnunuzi  na kupata elimu na namna ya kufanya kilimo.   

“Mifumo hii inasaidia wakulima kuwa na umoja wa kuweka mazao ghalani, kupata masoko rasmi, kufanya kazi na wafanya biashara rasmi, na kupata mikopo rasmi kutokana taarifa zao kuwa rasmi ,” na mifumo hii inawakaribisha wakulima na wafanya biashara kufanya kazi pamoja, aliongeza kusema,Bw. Mushi.

Pia aliipongeza Farm Africa kwa kuandaa warsha hiyo ambayo iliwakutanisha wakulima, mifumo ya mitandao hiyo na wadau wengine kujadili njia za kusaidia wakulima wadogo wa kilimo cha nafaka kujinasua toka katika vipato duni kutokana na mfumo holela wa masoko.

Farm Africa ni shirika linalounganisha biashara nzima ya nafaka kutoka kwenye shamba hadi sokoni na inashirikisha mkusanyiko wa program zinazoruhusu watumiaji kusimamia hesabu, mazao ya biashara, soko endelevu na kupata mkopo kutoka taasisi za fedha.

Warsha hiyo iliandaliwa na Farm Africa na kushirikisha wadau wa ndani ya nchi, Uganda na watu kutoka serikalini.
 Mkurugenzi wa Msaidizi Kitengo cha Kuzuia Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno Wizara ya Kilimo, Bi. Josephine Omolo kushoto akifuatilia mada katika warsha iliyokuwa ikizungumzia jinsi wakulima wanavyoweza kutumia mifumo ya mitandao kupitia simu za mkononi kutangaza bei ya mazao yao na kupata taarifa za kilimo bora na kipato chenye tija kuwawezesha kuondokana na hali duni katika familia zao, katikati ni Meneja Program ya FoodTrade wa Shirika la Kimataifa la Farm Africa,Bi. Beatrice Muliahela na kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo Vijijini na Mijini (RUDI), Lameck Kikoka.
 Wadau wa Shirika la Kimataifa la Farm Africa wanaojihusisha na shughuli za kilimo wakifuatilia  mada katika warsha iliyokuwa ikizungumzia jinsi wakulima wanavyoweza kutumia mifumo ya mitandao kupitia simu za mkononi kutangaza bei ya mazao yao na kupata taarifa za kilimo bora na kupata kipato chenye tija kuwezesha kuondokana na hali duni katika familia zao. 
Meneja Program ya FoodTrade wa Shirika la Kimataifa la Farm Africa,Bi. Beatrice Muliahela akifafanua jambo katika warsha iliyokuwa ikizungumzia jinsi wakulima wanavyoweza kutumia mifumo ya mitandao kupitia simu za mkononi kutangaza bei ya mazao yao na kupata taarifa za kilimo bora kupata kipato chenye tija na kuondokana na hali duni katika familia zao, katikati ni Mkurugenzi wa Msaidizi Kitengo cha Kuzuia Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno Wizara ya Kilimo, Bi. Josephine Omolo na kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo Vijijini na Mijini (RUDI), Lameck Kikoka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad