HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 28 February 2018

SERIKALI YASHAURIWA KUISHIRIKISHA MAHAKAMA KWENYE UANZISHWAJI WA MIKOA NA WILAYA

Na Lydia Churi-Mahakama, Kigoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Serikali kuishirikisha Mahakama ya Tanzania kwenye mipango yake ya uanzishaji wa maeneo mapya ya kiutawala ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake mjini Kigoma, Jaji Mkuu amesema mipango ya Serikali ya uanzishwaji wa wilaya au mikoa izingatie pia uanzishwaji wa Mahakama. Aliongeza kuwa Mikoa na wilaya mpya ndizo zenye ukosefu wa Mahakama hali inayowafanya wananchi kufuata mbali huduma za kimahakama.
Alisema Mahakama kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16 hadi 2019/20) imejipanga kutatua tatizo la ukosefu wa huduma za Mahakama pamoja na kusogeza huduma hizo karibu Zaidi na wananchi. Kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, tayari imeanza ujenzi wa Mahakama tano za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Manyara pamoja na ujenzi wa Mahakama 16 za wilaya na Mahakama Kuu mbili katika Mikoa ya Kigoma na Mara.
Jaji Prof. Juma amesema kupitia ziara yake ya siku saba kwenye Mahakama Kuu kanda ya Tabora amebaini kuwa watanzania wengi hufuata mbali huduma za Mahakama na maeneo mengine ni kutokana na jiografia ya maeneo hayo. Akitolea mfano wa wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Jaji Mkuu amesema kutokana na wilaya hiyo kuzunguka mkoa, wananchi wake hulazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu zilizopo umbali wa Zaidi ya kilometa 377.
Alisema Mahakama itaanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) kwenye maeneo yote yenye changamoto kama hizo kabla ya kujenga Mahakama kwa kuwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za kimahakama bado ni kubwa nchini.   
Kuhusu utendaji kazi, Jaji Mkuu aliwapongeza watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Tabora kwa kubuni mkakati wa kupunguza mlundikano wa kesi kwenye Mahakama zake. Kanda ya Tabora ndiyo kanda pekee nchini iliyopunguza siku za mpango wa upimaji wa kumaliza mashauri Mahakamani kutoka miaka miwili mpaka moja kwa kesi za Mahakama Kuu, miezi sita badala ya 12 kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na wilaya na kutoka miezi 6 mpaka 3 kwa kwa Mahakama za Mwanzo.
Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba 2017, kanda ya Tabora ilisajili jumla ya mashauri 1112 na mashauri yaliyosikilizwa na kumalizika yalikuwa 1194 wakati mashauri yaliyobaki Desemba 2016 yalikuwa ni 541.
Aidha Kanda ya Tabora imemaliza mashauri ya mlundikano kwa kiasi kikubwa hivyuo kufanya mashauri hayo kwisha kabisa katika Mahakama za Mwanzo na kupungua kwa kiasi kikubwa katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya. Mashauri ya mlundikano yaliyobaki Mahakama Kuu hadi kufikia Desemba 31 yalikuwa 4.
Kati ya mashauri hayo, mashauri yenye umri kati ya miezi 25-48 Mahakamani yalibaki 3 na shauri moja (1) lenye umri wa miaka 5-10 lilibakia. Aidha, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora haina mashauri yenye umri wa Zaidi ya miaka 10.
Jaji Mkuu amemaliza ziara yake ya siku saba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora ambapo alikagua shughuli mbalimbali za Mahakama pamoja na kuwatembelea baadhi ya wadau wa Mahakama wakiwemo wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kujadiliana na viongozi hao namna ya kupunguza changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau hao. 
  Jaji mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa pamoja na wakandarasi wa kampuni ya Masasi Contruction Ltd wanaojenga jengo la mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma. mahakama ya Tanzania inajenga jengo hili pamoja na mengine nchini ili kusogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi.
Jengo la mahakama kuu kanda ya Kigoma likiwa limefikia hatua hiyo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad