HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 1, 2018

DK.MPANGO ,MKURUGENZI BENK YA BARCLAYS WATETA UJENZI RELI YA KISASASA,MRADI UMEME WA STIGLER'S GORGE

Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amekutana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Kanda ya Afrika, Bw. Peter Matlare na kuiomba Benki hiyo kuangalia uwezekano wa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa viwango vya kimataifa (SGR) mradi wa miundombinu ya umeme wa Stieglar's Gorge ili kurahakisha maendeleo ya kiuchumi kupitia viwanda.

Amemweleza kiongozi huyo kwamba Serikali imeimarisha uchumi Mkuu kwa kudhibiti mfumuko wa bei ambao uko katika kiwango chatarakimu moja cha wastani wa asilimi 5.3 katika kipindi cha miezi 6 iliyopita.

"Tumewekeza kwenye miundombinu kama vile Elimu, maji, kilimo, afya, madini, na biashara na kwamba katika kipindi kifupi cha miaka 2 zaidi ya viwanda 80 vimejengwa katika eneo la Mkuranga mkoani Pwani, kutokana na fursa za uwepo wa bomba la gesi na eneo hilo kuwa karibu na Bandari ya Dar es Salaam.

Dkt. Mpango ameelezea pia mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) ambao amesema utarahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo katika nchi zinazopakana na Tanzania hivyo kukuza biashara kwa kiwango kikubwa.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika Bonde la mto Rufiji (Stiegler's Gorge), Dkt. Mpango amesema lengo la mradi huo utakao zalisha megawati 2,100 za umeme utakao kuwa wa uhakika na bei nafuu ili kukuza viwanda.

Alisema kuwa mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa kila biadhaa zinazozalishwa nchini pamoja na madini, vinaongezwa thamani hapa hapa nchini badala ya kuuzwa kama malighafi na kwamba nishati ya umeme ndiyo nguzo kuu ya kufikia malengo hayo.

"Ili tuweze kufikia azma hiyo tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika na wa bei nafuu ili viwanda vyetu viweze kuzalisha kwa wingi ndio maana tunaiomba Benki yako iweze kufikiria namna ya kushiriki katika ujenzi wa miradi hii" Alisisitiza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango ameipongeza Benki ya Barclays ambayo pia ni mwanahisa katika Benki ya NBC kwa ahadi yake ya kutaka kuwekeza kiteknolojia katika sekta ya benki nchini hatua ambayo itasaidia kukuza mitaji na mikopo kwa kundi kubwa la watanzania wakiwemo wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa.

Alielezea msimamo wake kwamba katika kukuza uchumi, Serikali inathamini mchango mkubwa wa Sekta Binafsi na imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba hivi karibuni alikuta na wadau wa Sekta ya Benki ili kusikiliza changamoto zao na pia kuwaeleza mambo muhimu ambayo ingependa sekta Binafsi ifanye ili kufikia malengo yanayokusudiwa.

Awali, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo ya Barclays anaye hudumia kundi la benki za Barclays Barani Afrika na kwingineko Marekani na Ulaya, Bw. Peter Matlare, ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kusimamia kikamilifu uchumi wa nchi unaokua kwa wastani wa asilimia 7.

Alisema hatua hiyo ni ya kupigiwa mfano katika nchi za Kiafrika na Duniani kwa ujumla ambapo amesema Tanzania imekuwa ikifanya vyema katika kukuza uchumi jumuishi unaowafikia watu wengi zaidi wakiwemo waishio mijini na vijijini.

Bw. Peter Matlare amemhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kwamba Benki yake itayafanyia kazi mapendekezo ya kutaka ushiriki wake katika ujenzi wa miradi mikubwa iliyoainishwa na Serikali kuwa kipaumbele chake.
 Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika Bw. Peter Matlare  akielezea umuhimu wa kushirikiana katika kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Benki yake wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.
 Ujumbe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), wakifuatilia mazungumzo kati yao na ugeni kutoka  Benki ya Barklays  nchini Afrika Kusini (hawako pichani), mkutano uliofanyika mjini Dodoma
 Ujumbe kutoka Benki ya Barclays uliongozwa na  Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika, Bw. Peter Matlare (kulia), wakichukua kumbukumbu wakati wa mkutano kati yao na  Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza wakati wa mkutano kati yake na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika, Bw. Peter Matlare (hayupo pichani), kuhusu namna ya kuboresha ushirikiano katika kukuza biashara kati ya Tanzania na benki yake, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.
 Maafisa Wakuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakichukua kumbukumbu wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika Bw. Peter Matlare (hawapo pichani), uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akipeana mkono na Makamu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika Bw. Peter Matlare, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tano kulia), Makamu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika Bw. Peter Matlare (wa sita kushoto) wakiwa katika picha yapamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Barclays baada ya kumalizika kwa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akiagana na Makamu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Afrika Bw. Peter Matlare, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Sera), Dkt. Khatibu Kazungu, akibadilisha mawazo na naimbu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays kundi la Afrika, Bw. Peter Matlare, baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya Wizara ya Fedha na Uongozi wa Beni hiyo kutoka Afrika Kusini, Mjini Dodoma

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad