HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 12 January 2018

WAWILI WAENDA JELA MIAKA 5 KWA KOSA LA KUSAFIRISHA DHAHABU

Na Karama Kenyunko, Glogu ya jamii.

WAFANYABIASHARA wawili maarufu Naushad Mohammed Suleiman (63) na Ali Makame Juma (36) wakazi wa Zanzibar, wamehukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya jumla ya sh.milioni sita baada ya kukiri mashtaka ya kusafirisha madini ya dhahabu vipande saba vyenye thamani ya Sh milioni 989.7 bila kuwa na leseni.

Hukumu hiyo imesomwa jana jioni na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mashauri amesema washtakiwa wametiwa hatiani kwa kukiri makosa waliyoshitakiwa nayo ya  uhujumu uchumi ambayo ni kula njama na kusafirisha dhahabu bila kuwa na kibali.
Aidha mahakama imeamuru kuwa, miche saba ya dhahabu pamoja na fedha za nchi 25 ambazo washtakiwa walikamatwa nazo zimetaifishwa na serikali.

Kabla ya kusomwa kwa adhabu, upande wa mashtaka ulitoa niche saba ya dhahabu, fedha za nchi 25 za kigeni zikiwa kwenye mabegi mawili.
 Kabla ya kusomewa adhabu mahakama iliuliza upande wa mashtaka kama wanalolote la kusema ambapo, Wakili  Faraja Nchimbi aliiomba mahakama itoe adhabu Kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwao na kwa wengine wenye mawazo ya kutenda kosa kama hilo.
Alisema vitendo vilivyofanywa na washtakiwa vinaleta hasara kubwa kwa nchi ya Tanzania na pia vinachangia kwa asilimia kubwa kurudisha nyuma uchumi wa Tainzania.
"Mheshimiwa ni rai yetu, washtakiwa wanastahili kupata adhabu Kali kwa mujibu wa sheria ili pia kulinda rasilimali za nchi yetu, amesema Nchimbi".

Katika utetezi wao washtakiwa wakiwakilishwa na Wakili wao Emmanuel Safari aliomba mahakama kutowapa washtakiwa adhabu Kali kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na pia wamekiri wenyewe kutenda makosa na wameondoa usumbufu wa kuita mashahidi kwani wamejutia makosa waliyotenda.
Aliongeza kuwa kitendo cha washtakiwa kuachia mali waliyokamatwa nayo ambayo ni mali halali inaonyesha kuwa  wameishajiadhibu. " Tunaomba mahakama izingatie kutokuwa na leseni ni suala ambalo wengi hawalijui hivyo wameishajiadhibu wenyewe" amedai Safari.
Ameongeza, mshtakiwa Mohammed ni mgonjwa hawezi kusimama vizuri pia anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

"Nimezingatia maombi ya upande wa mashtaka na uteezi wenu kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza lakini kitendo mlichofanya ni kosa na kinafanya uchumi wa nchi hii udidimie"

" Mahakama inawahukumu katika shtaka la kula njama kulipa faini ya sh.milioni mbili au kwenda jela miaka miwili na katika shtaka la pili la kusafirisha dhahabu mnatakiwa kulipa faini ya sh.milioni nne na mkishindwa mtatumikia kifungo cha miaka mitatu jela, na ikiwa mtaenda gerezani adhabu zote zitaenda pamoja", alisema Hakimu Mashauri.

Mapema jana asubuhi, wakati kesi hiyo ilipokuja kutajwa, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Jehovaness Zacharia ulidai mahakani hapo kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ametoa kibali cha kuipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri aliutaka upande wa mashitaka kuwasomea makosa upya ambapo wakili Zacharia alidai kuwa washitakiwa wanakabiliwa na makosa mawili, ambapo inadaiwa kati ya November Mosi na 29, 2017 katika siku isiyofahamika kati ya Dar es Salaam na Mkoa wa Geita, walikula njama kufanya kosa la kusafirisha madini nje ya nchi isivyohalali.

Pia wanadaiwa November 29, 2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume, walikutwa wakisafirisha madini  kwenda Dubai katika Falme za Kiarabu ambavyo in vipande saba vya dhahabu vyenye uzito wa kilogramu 18.354 vyenye thamani ya Sh. milioni 989.7 bila kuwa na leseni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad