HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 11 January 2018

WANAFUNZI WANAOJITOLEA KUFUNDISHA WAIOMBA SERIKALI KUWASAIDIA

   Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE), wanaotumia muda wao wa ziada kujitolea kufundisha katika shule za Msingi na Sekondari wameiomba Serikali kuwapa ushirikiano ili waweze kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwanzilishi na Mratibu Mkuu wa zoezi hilo, Emijidius Cornel alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na kazi hiyo wanayoifanya hususani katika Wilaya ya Temeke.

Cornel amesema kuwa wameamua kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano katika kuendeleza sekta ya elimu nchini kwa kujitolea kufundisha masomo ya sayansi na hesabu katika shule mbalimbali ili waweze kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuyapenda, kuyasoma na kuyapa kipaumbele masomo hayo.

“Tumeamua kutumia muda wetu wa ziada kuwafundisha wadogo zetu nao waweze kufikia au kuzidi tulipokuwa sisi lakini tunakumbwa na changamoto nyingi hasa nauli za kutufikisha na kuturudisha vyuoni kutoka katika shule tunazojitolea kufundisha hivyo tunaiomba Serikali na wadau wengine kutusaidia katika hili,”alisema Cornel.

Cornel ameongeza kuwa kwa yeyote atakayekuwa tayari kuwawezesha fedha kwa ajili ya nauli atume katika akaunti ya NMB ya Shule ya Sekondari Kibasila ambayo ni moja ya shule wanayojitolea kufundisha kwa namba 20701100005.

Mmoja wa wanafunzi wanaojitolea kufundisha, Nambo Nicodemu ametoa rai kwa wanafunzi wenzie wa vyuo vyote nchini kujenga tabia ya kujitolea katika shughuli mbalimbali zitakazoiletea nchi maendeleo.

“Kama Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli anavyosisitiza wananchi kufanya kazi kwa uzalendo basi tunaomba vijana wenzetu kujitolea kwa wingi kushirikiana na Rais katika kuendeleza gurudumu la maendeleo.” alisema Nicodemu.

Jumla ya wanafunzi 400 kutoka DUCE wanaojitolea walianza kazi hiyo mwezi Februari mwaka 2017, wanafundisha katika shule 10 zilizopo jijini Dar es Salaam na wana mpango wa kuendelea kujitanua katika shule nyingi zaidi.
Mratibu wa Walimu wa Kujitolea Manispaa ya Temeke, Emijidius Cornel akizungumza na waandishi habari kuhusu huduma wanayofanya katika kujitolea ya kufundisha wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad