HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 10, 2018

JKCI YAWAAHIDI WATANZANIA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA

Na Mwandishi Wetu, 
09/1/2018 Uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umewaahidi watanzania kuendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa kiwango cha kimataifa  kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. 
Ahadi hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na wakurugenzi wa Idara na vitengo vinavyojitegemea katika kikao cha kwanza cha Menejimenti  kwa mwaka 2018.
Prof. Janabi ambaye  pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho alizitaja ahadi zingine ni pamoja na kuendeea kupunguza kupeleka wagonja nje ya nchi, kupunguza gharama za tiba, kuongeza idadi ya huduma, kuboresha usafi katika Hospitali na kuendelea  kushirikiana na wananchi.

Mwenyekiti huyo alisema kwa mwaka 2018 wamejipanga  kutoa huduma kwa wagonjwa wengi zaidi ukilinganisha na mwaka jana ambapo jumla ya wagonjwa 64,093 walitibiwa katika Taasisi hiyo kati ya hao wagonjwa wa nje walikuwa 60796  na waliolazwa 3297.
“Malengo tuliyokuwa nayo kwa mwaka huu wa 2018 ni kuona wagonjwa wengi zaidi ya hawa tuliowaona mwaka 2017 katika kliniki zetu za kila siku. Taasisi imejipanga kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 400 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 1000.Tunatarajia kuwa na kambi maalum za upasuaji wa moyo  zisizozidi 15”. 

 “Mwezi huu tunatarajia kuwa na kambi mbili zote ni za upasuaji wa bila kufungua kifua. Tunaanza na kambi ya watu wazima  kwa kushirikiana na Taasisi ya Madaktari Afrika ya nchini Marekani.  Mwisho wa mwezi  tutakuwa na kambi ya watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart-SACH) ya nchini Israel”,  alisema.
Kwa upande wa viongozi waliohudhuria mkutano huo Prof. Janabi aliwataka kuwasimamia  wafanyakazi wanaowaongoza ili waweze kufanya kazi  zao kwa ufanisi na uweledi huku wakifuata maadili ya watumishi wa Umma hii itawafanya wananchi waweze kupata huduma bora zaidi.
Nao viongozi waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa watahakikisha wanafanya kazi zao kwa kujituma, kufuata kanuni za kazi  na kuwasimamia wafanyakazi wanaowaongoza ili wananchi waweze kunufaika na matibabu ya moyo yanayotolewa katika Taasisi hiyo.
Kwa mwaka 2017 jumla ya wagonjwa  1025  walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua katika Taasisi hiyo ambapo  zaidi ya bilioni 29 (Tshs. 29,725,000,000/=) ziliweza kuokolewa kama wagonjwa hao wangetibiwa  nje ya nchi. Gharama za mgonjwa mmoja anayetibiwa nje ya nchi ugonjwa wa moyo ni zaidi ya milioni 29.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiongea na wakurugenzi wa Idara na vitengo vinavyojitegemea kuhusu mikakati ya utendaji kazi kwa mwaka 2018 moja ya mkakati huo ukiwa ni kuendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa kiwango cha kimataifa  katika kikao cha kwanza cha Menejimenti  kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni Mwanasheria wa Taasisi hiyo Maulid Kikondo. 
 Wakurugenzi wa Idara na vitengo vinavyojitegemea vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi (hayupo pichani) alielezea kazi zilizofanyika katika Taasisi hiyo kwa mwaka 2017  katika kikao cha kwanza cha Menejimenti  kilichofanyika hivi karibuni. Jumla ya wagonjwa  1025  walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kwa mwaka 2017 na hivyo Taasisi kuokoa  zaidi ya bilioni 29 ambazo Serikali ingezilipa kama wagonjwa hawa wangefanyiwa upasuaji wa moyo nje ya nchi.
 Kikao cha kwanza cha Manejimenti  cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mwaka  2018 kikiendelea.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge akisoma  taarifa za utendaji kazi wa idara yake kwa kipindi cha miezi mitatu katika kikao cha kwanza cha Menejimenti kwa mwaka 2018 kilichofanyika hivi karibuni. Picha na JKCI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad