HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 15, 2017

WAZIRI LUKUVI AMALIZA MGOGORO WA ARDHI ULIODUMU MIAKA 10 CHAMWINO MKOANI DODOMA

WAZIRI wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi amefuta uamuzi wa viongozi wa Vijiji vya Membe na Mlimwa vilivyopo Kata ya Membe Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma wa kumpatia ardhi yenye ukubwa wa ekari 1756 mwekezaji David Mazoya Poli takribani miaka 10 iliyopita hali iliyosababisha mgogoro wa ardhi na kuhatarisha amani katika Kata hiyo.

Hali ya sintofahamu iliwagubika wakazi wa Kata hiyo kwani licha ya kukataa kutoa ardhi yao kwa mwekezaji huyo kupitia mikutano mikuu ya Vijiji, viongozi wao walimmilikisha Mwekezaji huyo ardhi hiyo  ikiwemo ekari 100 alizopewa na Kijiji cha Membe kwa makubaliano kuwa atawajengea Ofisi ya Serikali ya Kijiji ahadi ambayo hata hivyo hajaitekeleza.

Akizungumza na wakazi wa Kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara jana, Waziri Lukuvi alisema kuwa amefuta maamuzi yote yaliyofanywa na Serikali za Vijiji hivyo kwani yalikiuka Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inayotoa mamlaka kwa Vijiji kumilikisha ardhi isiyozidi ekari 50 tu na sio vinginevyo.

“Kuanzia leo nimefuta maamuzi yote yaliyofanywa na viongozi wa Vijiji hivi kumpa mwekezaji huyu ardhi yenye ukubwa wa ekari 1756 kwani ni kinyume cha Sheria ya Vijiji…hata kama Vijiji vitakubali kutoa ardhi kupitia mikutano mikuu ya Vijiji bado maamuzi hayo hayatakuwa halali endapo ardhi inayotolewa itazidi ukubwa wa ekari 50” alifafanua Waziri Lukuvi.

Alimtaka Mwekezaji huyo ambaye alifika katika mkutano huo, kufuata taratibu za kumilikishwa ardhi inayozidi ukubwa wa ekari 50 endapo ana nia ya kuendelea kuwekeza katika Kata hiyo, ikiwa ni kuomba ardhi katika Vijiji hivyo na endapo vitaridhia, vitapendekeza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwenye Mamlaka ya kumilikisha ardhi inayozidi ekari 50 baada ya ardhi hiyo kuhama kutoka katika Mamlaka ya Vijiji.

Wakazi wa Kata hiyo walimshukuru Waziri Lukuvi kwa uamuzi huo wa Serikali kwa madai kwamba wameteseka kwa kipindi kirefu ikiwa ni pampoja na kukosa maeneo ya kulima na malisho kwa ajili ya mifugo yao.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.  William Lukuvi akizungumza wakati wa Mkutano wa Hadhara katika Kata ya Membe Wilayani Chamwino jana ambapo alitoa uamuzi wa kuirudisha kwa Wananchi wa Vijiji vya Membe na Mlimwa ardhi yenye ukubwa wa ekari 1756 aliyepewa mwekezaji Davidi Mazoya Poli ( aliyesimama kushoto) kinyume cha taratibu miaka 10 iliyopita.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Membe wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi  alipofanya ziara katika Kata hiyo jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad