HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 22, 2017

WAKULIMA 14 WA PAMBA WAINGIA MATATANI WILAYANI IGUNGA KWA KUVUNJA SHERIA YA PAMBA.

WATU 14 wilayani Igunga wamekamatwa na Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa tuhuma za kukaidi maagizo ya kuwataka kulima pamba kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha pamba na kujikuta wakivunja Sheria ya Pamba ya mwaka 2001 na kanuni zake.

Watu hao walikamatwa hivi karibuni na Uongozi wa Wilaya ya Igunga kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri.

Alisema kuwa watuhumiwa hao walikutwa katika mashamba yao ya pamba wakiwa wamepanda pamba kwa mtindo wa kizamani ambao hauzingatia Sheria ya Pamba ya 2001 wengine wameacha maotea ambalo ni kosa.

Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa Mkoa aliwaagiza Maofisa Ugani wote kukagua shamba yote ili kujiridhisha kama wakulima waliobaki wamezingatia ulimaji wa kufuata Sheria na endapo watabainika kuwepo na waliokiuka wachukuliwe hatua haraka.

Alisema kuwa endapo atakuta katika eneo la Ofisa Ugani alilopangiwa kukagua mashamba kuna mkulima amelima bila kuzingatia Sheria na hajachukuliwa hatua itabidi amfukuze kazi.

Awali Katibu Tawala wa Wilaya ya Igunga Godslove Kawishe alisema kuwa wakulima walikamatwa kwa tuhuma za kukutwa wamepanda pamba kwa kurusha rusha mbegu ovyo bila kuzingatia matakwa ya kupanda kwa mistari na wengine walikutwa wameacha maotea yakiwa yameota na yamechanganyikana na shamba la mahindi.

Alisema kuwa miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji na Vitongoji ambao ndio waliokuwa wakituhumiwa kwa kosa la kushindwa kusimamia hadi wakulima kulima bila kuzingatia Sheria.

Kawishe aliongeza kuwa hata walipokuwa wakiombwa taarifa za wakulima wao walikuwa hawatoi ushirikiano kwa maafisa Ugani wa eneo husika.

Sheria ya Pamba 2001  na Kanuni zake za mwaka 2011 sehemu ya tatu katika kipengele cha 12 kinakataza kulima bila kuzingatia kanuni za kilimo bora, kipengele cha 13 kinakataza kuchanganya pamba na mazao mengine na kipengele cha 14 kinakataza kuacha maotea.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo Bodi ya Pamba imepewa mamlaka ya kuharibu shamba kwa gharama za mkulima pia mkulima anayebainika na kosa hilo atahukumiwa kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja au kifungu kisichopungua  miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad