HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 1 December 2017

NAIBU WAZIRI NISHATI SUBIRA NA NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI ULEGA WAZINDUA UMEME WA NISHATI YA JUA KISIWA CHA KWALE


Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Mb) Mkuranga Abdallah Ulega wakikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa mradi wa umeme wa nishati yajua uliojengwa na kampuni ya TANDEM kwa ufadhili wa Wakala wa umeme wa Vijijini REA, uzinduzi ulifanyika jana katika Kisiwa cha Kwale kata ya Kisiju Mkoa wa Pwani.


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
NAIBU waziri wa Nishati Subira Mgalu na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega wamezindua umeme wa nguvu za jua (Solar Power) katika Kisiwa cha Kwale uliojengwa na kampuni ya TANDEM na kufadhiliwa na wakala wa umeme Vijijini (REA).

Umeme huo uliogharimu takribani Milion 230 za kitanzania uliweza kuzinduliwa jana na Waziri wa Nishati sambamba na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo wa umeme wa nguvu za jua (solar power) kwa kisiwa cha Kwale kilichopo Kata ya Kisiju, Naibu Waziri wa Nishati Subira alisema kuwa hiyo ni moja ya hatua kubwa sana katika Kisiwa hicho ukizingatia umeme wa Tanesco unaoutumia nguzo hautaweza kufika kwa urahisi.

"Hii ni moja ya hatua kubwa sana kwa kijiji cha Kwale kwani walikaa kwa muda mrefu sana bila ya kuwa na nishati ya umeme na hasa ukiangalia changamoto iliyopo ni kuwa umeme wa Tanesco unaotumia nguzo usingeweza kufika huku, na sio huku tu hata visiwa vingin vya karibu na hapa ikiwemo Koma,"amesema Subira.
Naibu waziri wa Nishati Subira Mgalu akiwasha kitufe cha umeme kuashiria kuanzia sasa umeme unawaka katika Kijiji cha Kwale kata ya Kisiju jana Mkoani Pwani.

Naibu Waziri wa Nishati alisema, anafahamu umeme huo unaopatikana kwa Megawat 5.4 bado hautoshi kwa wanakijiji wote wa Kwale kwahiyo ombi lao la kutaka waongezewe bajeti ya kununua Panel za umeme ili kuweza kupatikana umeme kwa watu wote ambapo amelipokea na kwakuwa ni waziri mwenye dhamana ya kutaka kuhakikisha wananchi wote wananufaika kwa kuwa na umeme atalifanyia kazi.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega akiwa mbele ya wananchi wake wa Kijiji cha Kwale alisema kuwa kupatikana kwa umeme katika Kisiwa cha Kwale kutaleta maendeleo kwa wananchi hususani kwa wavuvi kwani samaki walikuwa wanaharibika kwa kukosa sehemu ya kuweka na kuishia kuharibika.

Alisema umeme huo utawasaidia wanakijiji wa Kisiwa cha Kwale na zaidi amewataka kuutumia kwa manufaa yatakayoleta tija maendeleo kwa kijiji kizima na cha zaidi ni kwenye kuinuka kiuchumi. Msafara wa viongozi hao uliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mkuranga Eng Mshamu Munde.

Wananchi wa Kisiwa cha Kwale wamefurahishwa sana na ujio wa umeme huo wa REA uliojengwa na TANDEM ambapo kwa miaka mingi sana wameshindwa kuwa na nishati ya umeme na kwa saaa hivi hata samaki wao wanauza kwa bei wanayotaka kutokana na kuwa na sehemu za kuhifadhia pamoja na mabarafu yanayouzwa kwa bei nafuu kabsa.

Mbali na hilo, mkandarasi wa wakala wa umeme wa Vijijini REA amefanikisha agizo la Naibu Waziri wa Nishati alilopewa siku ya Jumatatu kuhakikisha umeme unawaka kabla ya Ijumaa katika kata ya Kisiju na Mkamba ambapo Naibu Waziri alifika na kuthibitisha kama agizo lake limefanya kazi na kusema kuwa REA awamu ya tatu wananchi wote watapata umeme kwa haraka zaidi .
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga akizungumza na wananchi wa kisiwa cha Kwale wakati wa uzinduzi wa umeme wa nishati ya jua uliojengwa na kampuni ya TANDEM kwa ufadhili wa Wakala wa umeme Vijijini REA.
Panel zinazotumika kwa ajili ya umeme wa nishati ya jua kisiwa cha Kwale.
Naibu Waziri Wa Nishati Subira Mgalu na Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi (Mb) Mkuranga sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga Eng. mshamu Munde wakiwasili katika Kisiwa cha Kwale jana.


Picha na Emmanuel Massaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad