HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 15, 2017

TMF YAIPATIA REDIO HABARI NJEMA YA MBULU, FEDHA ZA RUZUKU YA SHILINGI MILIONI 112

Tanzania Media Foundation (TMF) imeipatia ruzuku ya shilingi milioni 112 Radio Habari Njema ya Mbulu Mkoani Manyara, kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi ili waibue kero, changamoto, mafanikio na kuandika kwa wingi habari za wananchi hasa waliopo Vijijini. 

Mkurugenzi wa TMF Ernest Sungura, akizungumza mjini Babati wakati wa zoezi hilo, alisema vyombo vya habari ni mhimili usio rasmi ambao umekuwa ukiibua changamoto mbalimbali za wananchi ikiwemo za maji, elimu, afya na mengineyo ambayo yakipatiwa ufumbuzi jamii inapata furaha. 

Sungura alisema kupitia ruzuku hiyo, hii ni mara ya nne kupatiwa ruzuku na TMF na mara zote wamekuwa wakiomba fedha kwa ajili ya kuandaa vipindi vyenye maslahi ya wananchi. 

Alisema kupitia vipindi vilivyoandaliwa na redio hiyo haki za watoto na wanawake zimepatikana kwa ufadhili wa TMF. 

Alisema kwa kuandika habari za jamii ikiwemo mafanikio, kero, ukosefu wa maji, vyoo, shule na mambo hayo yakapatiwa ufumbuzi wananchi hupata furaha baada ya mafanikio hayo. 

Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga ameipongeza TMF kwa kuiwezesha Redio Habari Njema, ambayo imekuwa inashirikiana na serikali katika kuchochea maendeleo ya jamii kupitia habari wanazozitangaza. 

Mofuga alisema kupitia redio hiyo wamekuwa wanapata taarifa za changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na wao kama serikali wamekuwa wanazifanyia kazi. 

Alisema waandishi wa habari wanapaswa kuiga chombo hicho cha habari kwa kutangaza mambo ya msingi ikiwemo kero za jamii na siyo kuegemea uandishi wa uchochezi usio na tija kwa jamii zaidi ya kuichonganisha na serikali yao. 

Alisema uandishi wa kuangalia maslahi ya Taifa ndiyo wa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia weledi na kuweka mzania ikiwemo kuandika taarifa za kumuunga mkono Rais John Magufuli. 

"Tuwe na uzalendo kwa kutambua juhudi za Rais Magufuli kwani amepambana na ufisadi, hivi sasa uadilifu umeongezeka, kero zilishamiri sasa zimepungua na amekuwa mlinzi wa rasilimali za Taifa," alisema Mofuga. 

Mhasibu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu, Padri Anthony Lagwen alisema tangu redio hiyo ianzishwe imekuwa nuru ya jamii kwenye eneo lote inaposikika. 

Padri Lagwen alisema kazi za redio hiyo zinalenga mafanikio kwa jamii na tangu wachukue ruzuku kwa mara ya kwanza mwaka 2012 wamepiga hatua kubwa kwa kuhabarisha jamii ipasavyo. 

Alisema kupitia mradi wa kwanza mwaka 2012 wa wanawake tuzungumze, walipata ruzuku ya sh42 milioni kutoka TMF na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia hadi kuheshimika na jamii. 
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga (kulia) akishuhudia utiwaji sahihi wa kupatiwa shilingi milioni 112 ambazo ni fedha za ruzuku kwa Redio Habari Njema ya Mbulu zilizotolewa na Tanzania Media Foundation (TMF) mjini Babati, (katikati) ni Mkurugenzi wa TMF Ernest Sungura na Mhasibu mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu, Padri Anthony Lagwen
 Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation (TMF) Ernest Sungura akizungumza mjini Babati wakati wa zoezi la kupatiwa fedha za ruzuku ya shilingi milioni 112 kwa Radio Habari Njema ya Wilayani Mbulu. 
 Mwandishi wa habari mwandamizi wa Mkoa wa Manyara, Joseph Lyimo akizungumza kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kuomba fedha za ruzuku Tanzania Media Foundation (TMF) Mjini Babati. 
 Waandishi wa habari wa Mikoa ya Manyara na Arusha, wakiwa kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kuomba fedha za ruzuku kupitia Tanzania Media Foundation (TMF) mjini Babati. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad