HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 15, 2017

KILIMO WATAKIWA KUTAFITI MBEGU BORA ZA PAMBA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni Mjini Dodoma kabla ya kikao kati ya Waziri Mkuu na Wabunge wanaotoka mikoa inayolima pamba Novemba 14, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokutana na wabunge wanaotoka mikoa inayolima pamba kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni mjini Dodoma Novemba 14, 2017. Kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya wabunge wanaotoka mikoa inayolima pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni mjini Dodoma Novemba 14, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wabunge kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma Novemba 14, 2017. Kutoka kushoto ni John Heche wa Tarime Vijijini, Marwa Ryoba wa Serengeti na Esther Matiko wa Tarime Mjini. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina ili kupata aina bora ya mbegu za pamba zitakazowanufaisha wakulima.



Amesema ni lazima utafiti huo ufanyike kwa kuzingatia aina ya udongo unaopatikana katika kila mkoa unaolima pamba.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Novemba 14, 2017) alipozungumza na wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima pamba, Bungeni mjini Dodoma.

“Mbegu za pamba ziko nyingi na zina migogoro. Mbegu nyingine zina manyoya, nyingine zina vipara hivyo lazima utafiti wa kina ufanyike ili kupata aina bora.”

Alisema Wizara ya Kilimo itumie taasisi zake vikiwemo vyuo kufanya uchunguzi na kubaini ni aina gani za mbegu zinafaa kutumika kulingana na eneo husika.

Alisema utafiti huo ambao utabainisha aina ya mbegu inayofaa kulingana na aina ya udongo katika kila eneo ili kumuwezesha mkulima kupata mazao ya kutosha.

Pia aliwataka Maofisa Kilimo katika mikoa inayolima mazao makuu ya biashara waweke kipaumbele katika kuyasimia mazao hayo.

Waziri Mkuu alisema Maofisa hao lazima wahakikishe wanayasimamia vizuri mazao hayo ambayo ni korosho, chai, pamba, kahawa na tumbaku ili yawe na tija.

Alisema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.

Waziri Mkuu alisema Serikali inataka kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.

“Tunataka kulifanya zao hilo ambalo lilikuwa likijulikana kama dhahabu nyeupe lifikie kiwango cha juu cha uzalishaji, hivyo kuongeza tija kwa wakulima.”

Pia Waziri Mkuu aliwaagiza Maofisa Kilimo katika mikoa hiyo wafanye sensa ili kutambua idadi ya wakulima wa pamba na ukubwa wa mashamba yao.

Alisema lengo la sensa hiyo ni kutambua idadi ya wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kurahisisha usambazaji wa pembejeo kulingana na mahitaji.

Wakizungumza katika mkutano huo baadhi ya wabunge waliiomba Serikali kuhakikisha zao hilo linaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuwafikishia wakulima pembejeo kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa Itilima Bw. Njalu Silanga aliiomba Serikali izibane Halmashauri ili kuhakikisha fedha za miradi ya kilimo zinatumika ipasavyo.

Bw. Silanga alisema msukumo wa Serikali wa kufufua zao la pamba umeanza kuzaa matunda, hivyo aliiomba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutafuta masoko ya kutosha.

Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Bi Ester Matiko ameiomba Serikali kuwaelimisha wananchi na kuwahamasisha kulima kilimo hicho ili waachane na kilimo cha bangi.

“Serikali ikitilia mkazo katika usimamizi wa mazao hayo tutasonga mbele na Tanzania ya viwanda tutaiona. Wakulima waelimishwe kuwa mazao hayo yana tija, hivyo wataachana na kilimo cha bangi.”

Bi. Ester alisema kati ya mazao makuu matano ya biashara manne yanalimwa katika jimbo lake ambayo ni chai, pamba, kahawa na tumbaku, hivyo wakulima wakipewa elimu ya kutosha juu za mazao hayo watapata tija.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, NOVEMBA 15, 2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad