HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 23, 2017

MHASIBU FEKI ATIWA MBARONI KWA WIZI WA TSH. 873,000

Na Nathaniel Limu, Singida
 Mhasibu wa hospitali ya mkoa mjini Singida aliyeachishwa kazi kwa kosa la kumiliki vyeti feki, Edith Talasi (49) mkazi wa Minga,anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kuvunja milango ya ofisi yake ya zamani na kuiba shilingi 873,000 taslimu, kwa kutumia funguo bandia.

Talasi  ambaye imelelezwa kwamba alifanya kazi hospitalini hapo kwa  muda na baadaye alirejeshwa kwenye kituo chake cha kazi manispaa ya Singida, kwenye wizi huo, alimshirikisha mlinzi wake wa nyumba ya kulala wageni Nandau, Antony Felix (51).Mlinzi huyo naye anashikiliwa na polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP Debora Magiligimba, alisema tukio hilo limetendeka Novemba, 21 saa 6.30 usiku huko katika hospitali ya mkoa mjini hapa.

Alisema siku ya tukio muuguzi wa zamu Shamir Omari (27) akitokea maeneo ya mapokezi akielekea wodini, alimwona mtu akiwa amesimama karibu na ofisi ya mhasibu, alisimama akamsalimia na mtu huyo aliondoka.

“Muuguzi huyo aliamini kuwa mtu aliyemwona,huenda alikuwa  mgonjwa au mtu aliyeleta mgonjwa hospitalini.Lakini aliporudi,alimwona mtu yule yule amerudi eneo lile lile, kitendo kilichopelekea amshuku kuwa sio mtu mzuri,” alisema kamanda huyo.

Alisema muuguzi huyo baada ya kumtilia shaka mtu huyo, alitoa taarifa kwa mlinzi wa zamu wa hospitali hiyo, Abubakari Jumanne,ambaye alimweka chini ya ulinzi mtu huyo.

ACP Magiligimba alisema hata hivyo mtu huyo alijitetea kuwa amefika hospitalini hapo, kwa ajili kuchoma sindano na kuonyesha dawa ya unga na kichanganyio chake.

“Wakati wanaendelea na mahojiano hayo,waliona makufuli  mawili ya mlango wa nje/grili yapo chini na mlango huo wa chuma upo wazi. Mtuhumiwa mlinzi Antony alieleza kuwa bosi wake (mtuhumiwa Edith) kwa wakati huo,alikuwa ndani ya ofisi ya mhasibu amejifungia ndani,” alisema.

 Akifafanua  alisema  jeshi la polisi baada ya kupata taarifa ya wizi huo, liliweza kufika eneo la tukio na kukuta mlango wa ndani ukiwa umefungwa kwa ndani.

“Walipoamuru mhasibu afungue mlango huo kwa kutumia funguo zake,walimkuta mtuhumiwa (Edith) akiwa amejibanza kwenye kona ya mlango na watumishi wa hospitali hiyo, waliweza kumtambua. Alipohojiwa ameingiaje humo ndani,alionyesha funguo saba (07) na zilipojaribiwa ziliweza kufungua milango yote ya ofisi ya mhasibu,” alisema Magiligimba.

Alisema pamoja na wizi huo wa shilingi 873,000,imeelezwa kwamba aprili mwaka huu,wahasibu wa hospitali hiyo,walibaini upotevu wa shilingi 1,800,000.Oktoba mwaka huu,pia walibaini upotevu wa shilingi 3,600,000.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. David Mwasita,amekiri kutokea upotevu huo lakini wahasibu katika wakati huo,waliweza kuziba upotevu huo, kwa fedha zao za mishahara.

Ameeleza kuwa wahasibu hao walilazimika kutoa fedha zao binafsi, na wasingeweza kutoa taarifa ya upotevu huo, kwa vile milango na kasiki, ilikuwa imefungwa kama kawaida.

ACP Magiligimba amesema kwa sasa wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo,watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad