HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 23 November 2017

Dkt. Mwakyembe afungua mashindano ya SHIMMUTA

Na Lorietha Laurence-WHUSM, Iringa.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe ameshukuru ushirikiano unaonyeshwa na Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kuunga mkono dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza na kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Waziri Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo jana kwenye kiwanja cha mpira wa miguu cha Samora Mkoani Iringa alipokuwa akifungua mashinadano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) ambapo aliwataka watumishi hao kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali iliyoanishwa.
“Michezo ni muhimu kwa afya na katika kujenga ushirikiano na urafiki ili kuleta matokeo bora na ufanisi wa kazi pale mnaporudi katika maeneo yenu ya kazi na jamii kwa ujumla” alisema Mhe.Dkt. Mwakyembe.
Aidha Waziri Dkt. Mwakyembe alieleza kutoridhishwa na baadhi ya Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kutokushiriki katika mashindano hayo kwa kutoa sababu mbalimbali.
“Nitamjulisha mlezi wa Kitaifa wa SHIMMUTA Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu changamoto zinazotokana na Mashirika na Taasisi za Serikali ambazo zumekuwa zikiacha kushiriki kwenye mashindano haya” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Masenza aliwahakikishia usalama, amani na ulinzi  washiriki wa mashindano hayo katika kipindi chote cha mashindano pamoja na huduma bora za kijamii.
“Tumefurahi mmechagua Mkoa wetu wa Iringa kwa ajili ya mashindano haya, nawasihi mkipata muda msiache kutembelea vivutio vya kitalii  na kihistoria vikiwemo maeneo ya Isimila, Kalenga na Hifadhi ya Ruaha” alisema Mhe. Amina Masenza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA Bw.Hamis Mkanachi alimuomba Waziri Mwakyembe kulisaidia shirikisho  hilo ili Mashirika na Taasisi za Seriklai zinazoshindwa kushiriki ziwezi kushiriki .
Bw. Mnachi aliongeza kwa kueleza kuwa kuna umuhimu wa SHIMMUTA kushirikiana kwa karibu na Shirikisho la upande wa Zanzibar ili kuwaleta pamoja  watumishi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kwa pamoja. 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wa tatu kushoto) akishangilia ufunguzi wa mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) jana mjini Iringa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad