HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 6 November 2017

Diwani wa CHADEMA Kihesa ajiuzulu, ajiunga CCM

Diwani wa Chadema Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa, Edgar Mgimwa amekihama chama hicho na kujiunga na CCM.
Mgimwa amejiondoa katika chama hicho wakati kukiwa na ushindani mkali kati ya Chadema na CCM katika uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye kata mbili mkoani Iringa unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017.
Alitangaza uamuzi huo jana Jumapili Novemba 5,2017 wakati wa mkutano wa kampeni za CCM katika Kata ya Kitwiru. Kata nyingine inayofanya uchaguzi ni Kimala iliyoko wilayani Kilolo.
Mgimwa ameungana na wenzake watatu waliohama Chadema miezi kadhaa iliyopita akiwemo Baraka Kimata anayewania tena udiwani katika Kata ya Kitwiru, safari hii kupitia CCM.
Wengine ni waliokuwa madiwani wa Viti Maalumu (Chadema), Leah Mleleu na Husna Daudi ambao baada ya kujiuzulu walisema wataendelea kuwa wanachama wa chama hicho.
Hata hivyo, katika mkutano wa kampeni wa CCM jana walitangaza kujiunga na chama hicho. Wanachama hao wapya walipokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.
Mgimwa akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Novemba 6,2017 amesema miongoni mwa sababu zilizomfanya ahame Chadema ni alichodai udikteta wa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Amesema kutokuwepo maelewano baina ya mbunge huyo na mmoja wa viongozi wa wilaya ya Iringa kunasababisha kuzorota kwa maendeleo jambo ambalo haliungi mkono.
Akizungumzia madai hayo, Mbunge Msigwa ameieleza Mwananchi kuwa, Chadema haibabaishwi wala kuyumbishwa na hatua ya diwani huyo kuhama.
Mchungaji Msigwa amesema chama hicho kina uhakika kuwa huo ni mwendelezo wa kile alichodai baadhi ya madiwani kununuliwa.
Amesema wanachokifanya sasa ni kujipanga kwenye uchaguzi mdogo ili kurejesha kata zilizokuwa zinashikiliwa na Chadema.
“Ukiwa vitani, inapotokea askari anaanguka huna haja ya kugeuka nyuma kwa sababu hafanyi jeshi zima kuyumba, sisi tunasonga mbele; na kwa sababu tunajua ni mpango wa kutengeneza hatuna wasiwasi katika hilo,” amesema Mchungaji Msigwa.
Amesema kwa sababu kata zinazoachwa wazi zitaitishwa uchaguzi mdogo, kazi yao itakuwa kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.
Kuhusu hilo, Katibu wa Itikadi, Hamasa na Uenezi wa CCM Manispaa ya Iringa, Edol Bashiri ameieleza Mwananchi kuwa wataendelea kuwapokea madiwani wengine wanaohamia chama hicho kwa kuwa milango ipo wazi.
“Wanafuata sera safi na demokrasia inayoendeshwa kwa vitendo, tunaendelea kuwakaribisha wengine wanaotaka kuja na tutaendelea kuwapokea,” amesema.
Bashiri amesema wanaendelea kufanya kampeni na kwamba, wapo wanachama wengine wanaohamia CCM wakitokea Chadema.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad