HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 6, 2017

ALIYEIPAISHA TUSIIME KITAIFA ATAKA KUWA DAKTARI WA MOYO

MWANAFUNZI Ibrahim Shaban wa shule ya Tusiime aliyeibuka mshindi wa kwanza kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa taifa kumaliza elimu ya msingi amesema ndoto yake ni kuwa daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo.

Akizungumzia namna alivyoyapokea matokeo hayo alisema, amefurahi sana na kuahidi kuendelea kufanya vizuri zaidi akiwa sekondari ili aweze kutimiza ndoto zake.

Alisema siri ya mafanikio yake ni jitihada kubwa za walimu wake akiwa shule ya msingi Tusiime na aliwamwagia sifa wazazi wake ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo yake ya klitaaluma siku hadi siku.

Ibrahim alisema kuwa ndoto yake ya muda mrefu ni kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo hivyo aliahidi kuwa atasoma kwa bidii hadi ahakikishe ndoto zake zinatimia.

 “Nawashukuru walimu wangu wa Tusiime maana tulikuwa tunasoma usiku na mchana, mafanikio haya hayajaja kwa kubahatisha bali ni jitihada kubwa zimefanyika, nawashukuru wazazi wangu na nawaahidi nitafanya vizuri zaidi hadi niwe daktari wa moyo,” aliahidi Ibrahim ambaye aliongoza kitaifa kwa upande wa wavulana na shule yake kuwa ya kwanza Wilaya ya Ilala na ya a tatu kwa Mkoa wa Dar es Salam.

Mama mzazi wa Ibrahim, Mery Semwenda alisema si mara ya kwanza kwa Ibrahim kupata matokeo mazuri kama hayo kwani aliwahi kuwa wa kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye matokeo ya darasa la nne.

“Akiwa darasa la nne hapo hapo Tusiime aliongoza katika matokeo ya darasa la nne kwa Mkoa wa Dar es Salaam na alipewa zawadi ya ngao na cheti na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick,” alisema

Alisema mazingira mazuri ya kusoma ya shule hiyo ndiyo yamekuwa yakisababisha wanafunzi wengi wa shule hiyo kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa kuanzia darasa la nne, la saba, kidato cha pili , cha nne na cha sita.

Alipoulizwa anamipango gani ya kuendeleza kipaji cha mtoto wake, aliiomba serikali iwatambue na kuwathamini,iwawezeshe na  iwawekee mazingira mazuri wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani yao.

“Serikali iwaweke pamoja wanafunzi wenye vipaji kama Ibrahim ili waendeleze vipaji vyao kwa faida ya taifa tofauti na sasa ambapo wanatangazwa tu kwenye magazeti lakini hakuna mfumo mzuri wa kuwafuatilia na kuendeleza vipaji vyao,” alisema na kuongeza

“Kwa mataifa mengine wanafunzi wenye vipaji kama hawa wanaangaliwa vizuri na kusaidiwa na serikali na mwishowe wanakuja kuwa wataalamu bingwa kwenye fani mbalimbali hivyo kutoa mchango wao kwa taifa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad